NAIBU WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR AMEWATAKA MAAFISA WA AFYA KUFANYA KAZI KWA BIDII

 Naibu Waziri Wizara ya Afya Hassan Khamis Hafidh akizungumza na Maafisa wa Afya kuhusu utendaji wa kazi, katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Jengo la kitengo shirikishi cha Kinga Mama na Mtoto huko Kidongo chekundu Mjini Zanzibar.

Naibu Waziri Wizara ya Afya  Hassan Khamis Hafidh amewataka Maafisa wa Afya kufanya kazi kwa bidii ili kuisaidia jamii kwa kuweka mazingira salama na kuepuka  maradhi ya mripuko.

Hayo ameyasema katika kikao cha maafisa wa Afya kilichofanyika  Ukumbi wa Jengo la Kitengo Shirikishi cha Kinga Mama na Mtoto Kidongo-chekundu Mjini Zanzibar.

Amesema Maafisa hao wanawajibu mkubwa wa kuisaidia adhma ya Serikali ili kuhakikisha Zanzibar inakua na mazingira safi na salama.

Aidha amewataka Maafisa hao kuwa wabunifu katika kusimamia kazi zao na kuhakikisha wanatoa huduma bora ili kuondosha usumbufu uliokuwa unalalamikiwa na jamii.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Maafisa wa Afya Abdalla Rashid ameahidi kuwa atayafanyia kazi na kuhakikisha wanafikia malengo yaliyokusudiwa .

Nao maafisa hao wameeleza kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika ufanyaji wa kazi zao ikiwemo usafiri pamoja na nyenzo za kufanyia kazi.

Loading