TUTAKABILIANA NA CHANGAMOTO KUJENGA ZANZIBAR NJEMA YENYE AFYA – MHE. OTHMAN

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kuwa Serikali haitosita kuchukua kila juhudi kwa kadiri itakavyowezekana, ili kuhakikisha ufumbuzi wa kero mbali mbali zinazoikabili Sekta ya Afya Nchini unapatikana.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo Maalum ya Uvimbe wa Ubongo na Saratani (Neuro–Oncology Brain Hemisphere Anatomy Through Clinical Cases), katika Hospitali ya Rufaa, Mnazi Mmoja jijini Zanzibar.

Amesema Serikali inaelewa uwepo wa changamoto ndani ya Sekta hiyo zikiwemo za kukosekana kwa baadhi ya vifaa, mapungufu katika Chumba cha Upasuaji, na uhaba wa wafanyakazi, hali inayosababisha kufanyika kwa idadi ndogo ya shughuli za upasuaji, chini ya kiwango ambacho kingelipendekezwa, bali ipo dhamiri ya kuzitatua ambapo juhudi za awali zimeanza.

Mheshimiwa Othman ametaja juhudi hizo kuwa ni pamoja na ukarabati wa majengo, uwekaji wa vifaa, sambamba na utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Mwinyi, ya kuajiri watumishi wa umma wapya wakiwemo wa kada ya afya.

Mheshimiwa Othman ameipongeza Taasisi ya Matatizo ya Vichwa, Migongo na Mishipa ya Fahamu (NED Institute), na pia juhudi zinazochukuliwa na Daktari Bingwa kutoka Spain, Profesa JOSE Piquer, na uongozi mzima wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kazi kubwa wanayoitekeleza licha ya mazingira hayo magumu.

Aidha ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo ya Siku Tatu (3) kujitahidi kuuthamini sana muda wao katika kujiongezea elimu, ujuzi, maarifa, na pia kuendeleza tabia ya kujifunza mara kwa mara, ili kujijengea uwezo wa kutoa huduma zilizo bora zaidi kwa wananchi, sambamba na kuweka azma ya utayari, kuwa makini, watulivu, wasikivu na hatimaye kuyapokea mafunzo hayo muhimu, ili kuijenga Zanzibar Njema yenye afya.

Naye, Waziri wa Afya, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, amewataka Madaktari, Wauguzi pamoja na Washiriki wa Mafunzo hayo kuwa wastahamilivu na kujitolea kwa moyo wote wakielewa kuwa Serikali inatambua juhudi na maslahi yao ambayo yatatekelezwa kikamilifu pindipo hali ya uchumi wa nchi, iliyoathiriwa na UVIKO-19 itakapotengamaa.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Daktari Bingwa kutoka Spain, Profesa JOSE Piquer amesema ni imani yake kuwa taaluma itakayopatikana hapo ni muhimu sana na yenye thamani kubwa, na ambayo yatasaidia sana, hasa kutokana na kuwashirikisha Mabingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Duniani.

Waliojumuika katika hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Afya, Mheshimiwa Hassan Khamis Hafidh, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dr. Msafiri Marijani, Wakurugenzi wa Huduma za Tiba na Huduma za Uuguzi, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mkuu wa Taasisi ya Matatizo ya Vichwa, Migongo na Mishipa ya Fahamu, Dokta Said Idrissa Ahmada, Waelekezi na Washiriki wa Mafunzo ambao kwa kiasi kikubwa ni Wauguzi na Madaktari Bingwa kutoka hapa Nchini.

Loading