MAFUNZO YA SIKU TATU KWA WATAALAM WA AFYA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUHUSU UGONJWA WA KISUKARI YAFUNGULIWA ZANZIBAR

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu matatizo ya miguu yanayotokana na ugonjwa wa kisukari (diabetic foot) kwa wahudumu wa afya wakiwemo madaktari wa upasuaji (Surgeons), watengeneza viatu (orthotic) na wauguzi kutoka hospitali mbalimbali za Rufaa, Kanda, Mikoa na Wilaya Tanzania bara na Zanzibar huko katika ukumbi wa Hotel ya Zanzibar Beach, Mazizini mjini Zanzibar

Wataalam na wahudumu wa afya wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa kisukari ili kupunguza wimbi la kukatwa Miguu kwa wagonjwa wa kisukari nchini

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matatizo ya miguu yanayotokana na ugonjwa wa kisukari (diabetic foot) kwa wahudumu wa afya wakiwemo madaktari wa upasuaji (Surgeons), watengeneza viatu (orthotic) na wauguzi kutoka hospitali mbalimbali za Rufaa, Kanda, Mikoa na Wilaya Tanzania bara na Zanzibar.

Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa madaktari na wauguzi wengine katika hospitali zao ili kufanya kazi kwa pamoja kuzuia matatizo yatokanayo na athari za ugonjwa wa kisukari.

Akielezea hali halisi ya Ugonjwa huo Naibu Waziri amesema Ripoti za kitaalam zinaeleza kuwa  watu million 537 wanaishi na ugonjwa wa kisukari duniani na milioni 24 ni kutoka katika nchi za kiafrika ambapo watu milioni 55 wanakadiriwa kuwa na ugonjwa wa kisukari kufikia mwaka 2045.

Ameongeza kuwa kila baada ya sekunde 30 mguu mmoja unakatwa kwa sababu ya tatizo la kidonda cha mguu wa kisukari(diabetic foot ulcer) duniani kote jambo ambalo pia husababisha kulazwa kwa wagonjwa hospitalini na kuigharimu serikali fedha nyingi za matibabu.

Ameushukuru uongozi wa Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA)  kwa kutafuta ufadhili wa mafunzo hayo na kuichagua Zanzibar kuwa kituo chao cha mwanzo kufundisha wataalamu  kutoka Hospitali za Rufaa, Mikoa, Kanda na Wilaya hasa baada ya kugundua kuwa wagonjwa wengi wa Diabetic foot wanatoka Zanzibar.

Awali akimkaribisha mgeni Rasmi Naibu mkurugenzi amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wahudumu hao kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa kisukari na kugundua mapema athari zitokanazo na ugonjwa wa kisukari zikiwemo matatizo ya miguu ili kupunguza tatizo linaloshamiri la kukatwa miguu.

Amesema kwa mujibu wa utafiti iliyofanyika mwaka 2011 (step survey) na tafiti ndogo iliyofanyika mwaka 2020 imeonyesha ugonjwa wa Kisukari unakuwa kwa asilimia 4% sawa na kusema kati ya watu 100 watu 4 wanaugua Ugonjwa wa Kisukari.

Ameongeza kuwa Tanzania inaweza kuondokana au kuupunguza ugonjwa wa Kisukari pale panapokuwa na mashirikiano na rasilimali za kutosha kukabiliana na tatizo hilo.

Akielezea vyanzo vikuu vya maradhi ya Kisukari Mwenyekiti Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) Andrea Swai amesema ni pamoja  mabadiliko ya mfumo wa Maisha,  urithi kutoka kwa familia, unene uliokithiri, utumiaji wa Tumbaku ikiwemo uvutaji wa sigara

Sababu nyingine ni pamoja na kutokufanya mazoezi, matumizi ya Pombe kupita kiasi na mlo usio kamili.

Mwenyekiti Swai amesema athari nyingi za Kisukari zinachangiwa kwa watu kuchelewa kujigundua mapema kuwa wana ugonjwa wa Kisukari na hata pale wanapojigundua baadhi ya wataalam wa afya huchelewesha kuwapa rufaa hivyo kupelekea kuishia kukatwa miguu.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika Zanzibar katika Ukumbi wa Hotel ya Zanzibar Beach mjini Zanzibar yamekuja kutokana na ongezeko kubwa la Wagonjwa wa kisukari kukatwa miguu huku idadi kubwa ya wagonjwa wa Kisukari nchini Tanzania ikiripotiwa wanatokea Zanzibar.

Loading