MAADHIMISHO YA SIKU YA FIGO DUNIANI YAFANYIKA ZANZIBAR

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk Fatma Mrisho akitoa hotuba ya Maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani yaliofanyika katika Uwanja wa Hospitali Mnazi Mmoja Zanzibar

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Fatma Mrisho amesema hospitali za kisasa zinazojengwa katika maeneo mbali mbali nchini zitakuwa na vitengo maalum vya kusafisha damu kwa wagonjwa wa maradhi ya Figo.

Akizungumza katika siku ya maadhimisho ya siku ya Figo duniani kwa niaba ya Waziri wa Afya amesema ugonjwa wa figo  ni hatari sana hivyo kuwepo kwa kitengo hicho kutasaidia kuondoa usumbufu wa wagonjwa kufuata huduma katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.

Aidha amesema kuwepo kwa kitengo hicho kitasaidia kuimarisha afya za wagonjwa kwani wanapata usumbufu mkubwa wakati wanapohitaji matibabu.

Nae Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Mnazi Mmoja Dkt Msafiri Marijani amesema endapo wananchi watabadilisha mtindo wao wa maisha kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya wanaweza kuepukana na maradhi tofauti.

Amesisitiza haja ya kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuweka miili sawa na kuepukana na maradhi nyemelezi.

Kuhusu tatizo la uhaba wa madaktari bingwa nchini dk. Marijani amewashauri wataalam na wasomi wa kada ya Afya kusomea fani muhimu ikiwemo upasuaji mishipa ya damu, moyo, figo ili kupunguza idadi ya kupeleka wagonjwa nje ya Zanzibar kupata matibabu.

Akisoma risala daktari bingwa wa ugonjwa wa figo dk.Mariam Hamad amesema wameandaa kampeni maalum ya kukabiliana na ugonjwa huo hatari ikiwemo kutoa elimu kupitia vyombo vya habari,vipeperushi na mikutano ya wananchi katika shehia mbali mbali nchini.

Aidha amesema kitengo chao kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa wafanyakazi, chumba cha upasuaji kwa ajili ya kusafishia damu na uwekaji vifaa pamoja na mafundi wa mashine zinapoharibika.

Siku ya figo duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 10 Machi ya kila mwaka ambapo kauli mbiu yake kwa mwaka huu ni “afya ya figo kwa wote”.

Loading