WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR AWASISITIZA WAZAZI KUWAPATIA CHANJO KAMILI WATOTO WAO

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui amesisitiza umuhimu kwa wazazi na walezi kuwapatia watoto wao chanjo kwani ni kinga kubwa ya maradhi yanayozuilika kwa njia hiyo.

Amesema chanjo ni muhimu kwa watoto katika kuimarisha makuzi yao na kuwafanya wawe na afya bora iwapo watapatiwa kwa ukamilifu na kwa wakati.

Waziri Mazurui ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa wiki ya chanjo Afrika ambapo kwa Zanzibar uzinduzi huo ulifanyika kituo cha afya cha Mwera, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amewataka wananchi wasipuuze kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kupatiwa chanjo kwani kinga ni bora na rahisi kuliko tiba.

Waziri wa Afya ameikumbusha jamii lengo la Afrika kuweka wiki maalumu ya chanjo kuwa ni kuwatanabahisha umuhimu wake na kutoa fursa kwa watoto waliofika umri wa kupata chanjo kupatiwa na ambao hawajakamilisha na umri wao hauzidi miaka mitano wapelekwe vituoni kukamilisha.

Aidha amewashauri wazazi wa kiume kuwapa ushirikianao wenziwao katika kufanikisha mpango wa chanjo kwa watoto wao kwani baadhi wameonekana kutowapa ushirikiano.

Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Hadid Rashid Hadid amesema wananchi wa Mkoa huo wanamuamko mkubwa katika suala la chanjo na kwa mujibu wa takwimu wanaoongoza kwa Mikoa yote ya Tanzania.

Amemuhakikisha Waziri wa Afya kwamba uongozi wa Mkoa huo utaendelea kusimamia na kufanya kila juhudi ili kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo kwani ni moja kati ya haki yao ya msingi.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amekiri kuwa wapo akinamama wachache ambao hawakamilishi chanjo kwa waoto wao na mkakati wa kuwahimiza  utawekwa ili wakamilishe na kuendelea kuwa mfano kwa Mikoa mengine.

Kaimu Daktari zamana kituo cha Afya Mwera Salma Bakari Muhd amesema kituo hicho kimekuwa kikifanya vizuri katika kutoa chanjo za watoto ingawa bado kuna baadhi ya akinababa wamekosa mwamko na kuhisi kuwa kazi ya kuwapeleka watoto vituo cha afya ni kazi ya akinamama peke yao.

Kaulimbiu ya wiki ya chanjo Afrika mwaka huu ‘Chanjo huweka jamii pamoja.’

Loading