ZANZIBAR YAADHIMISHA SIKU YA MALARIA DUNIANI

Imeelezwa kuwa kiwango cha maradhi ya Malaria Zanzibar sio cha kutisha lakini juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha lengo la kuyaondosha kabisa maradhi hayo linafikiwa.   

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana alieleza hayo katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni.

Amekumbusha kwamba mwaka uliopita watu 20 waliripotiwa kufariki dunia kutokana na kuugua maradhi ya malaria hali inayoonyesha kuwa bado maradhi yaho yapo Zanzibar.

Alieleza kuwa suala la kuimarisha usafi wa mazingira, kuondosha mazalio ya mbu, matumizi sahihi ya vyandarua vilivyotiwa dawa na kupiga dawa sehemu ambazo  maradhi hayo yanaendelea kujitokeza ni miongoni mwa mikakati ya kuondosha kabisa.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Mgharibi alisema takwimu zinaonyesha wagonjwa wengi waliougua malaria katika miaka ya karibu ni waliotoka nje ya Zanzibar ama wenye tabia ya kusafiri mara kwa mara.

Amewashauri wananchi watakaojihisi wanadalili za kuugua malaria kuwahi vituo vya afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ili yasiweze kusambaa zaidi kwa wananchi wengine.

Akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika hilo Zanzibar  Dk. Ghirmany Andermaechal amesema maradhi ya Malaria yanaendelea kuwasumbua wananchi wengi katika Bara hilo na kupelekea vifo vingi.

Ametaka mashirikiano ya pamoja baina ya wananchi, wadau mbali mbali na mashirika ya Kimataifa katika kukabiliana na maradhi hayo ili kuhakikisha hayasumbui wananchi.

Kaulimbiu ya siku ya Malaria Duniani mwaka huu ‘Tumia chandarua kilichotiwa dawa kitatukinga na Malaria.’        

Loading