RAIS DK.MWINYI AFUNGUA MKUTANO MKUU WA MADAKTARI WA UPASUAJI TANZANIA (TSA)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa bado kuna kazi kubwa inayohitaji kufanywa ili kuwa na wataalamu wa kutosha hasa katika utoaji wa huduma za upasuaji.
 
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahr Bweni, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA).
 
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa mara nyingi wagonjwa wanaohitaji huduma za upasuaji hulazimu kuwapatia rufaa nje ya nchi, jambo ambalo lina gharama kubwa kwa Serikali na lenye kuleta usumbufu kwa wagonjwa na wanafamilia wanaouguliwa.
 
Aliongeza kuwa ikiwezekana kuwa na wataalamu wa kutosha wa upasuaji kwa maradhi mbali mbali yanayowasibu wananchi itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji katika sekta ya afya ambazo hadi sasa ni kubwa.
 
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali zote mbili zinahitaji kuwa na mikakati imara ya kupunguza upelekaji wa wagonjwa nje ya nchi ili kupunguza gharama ambapo alitolea mfano kwa upande wa Zanzibar katika kipindi cha Julai mwaka 2019/2020, jumla wagonjwa 726 walipatiwa rufaa nje ya Zanzibar na matibabu yao yaligharimu TZS  Bilioni 8.
 
Aidha, alisema kuwa kwa mwaka uliofuata Julai 2020 hadi Juni 2021, jumla ya wagonjwa 239 walipatiwa rufaa nje ya Zanzibar na matibabu yao yaliigharimu Serikali jumla ya TZS  Bilioni 3.7 idadi ya wagonjwa kwa mwaka huo imeshuka kutokana na kuzuia wagonjwa kusafiri nje ya nchi kwa sababu ya mripuko wa ugonjwa wa Korona.
 
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana bado sekta ya afya imekabiliwa na changamoto nyingi katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Alisema kua ushauri wao unahitajika juu ya namna bora ya kuimarisha miundombinu na mifumo ya afya ili kuweza kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo nchini.

Loading