WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR WATAKIWA KUPIGA VITA MATUMIZI YA SIGARA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia, na Watoto Dk. Omar Dadi Shajak ameitaka jamii kuacha kutumia bidhaa zinazotokana na tumbaku kwani ni kichocheo kikubwa cha maradhi yasiyoambukiza ambayo yamekuwa  tishio kubwa duniani.

Akifungua mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu Kanuni ya tumbaku ya mwaka 2016 Ofisini kwake Mnazimmoja, amesema matumizi ya tumbaku yamekuwa yakipoteza maisha ya watu wengi hivi sasa.

Katika kupiga vita matumizi ya tumbaku, Dk. Shak amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwatuma watoto dukani kununua sigara kwani kufanya hivyo ni kuwahamasisha kuingia katika mkumbo wa kuvuta sigara.

Katibu Mkuu Shajak amewashauri wavutaji wa sigara kufuata Kanuni ya tumbaku kuacha kuvuta sigara katika mikusanyiko ya watu kwa lengo la kuwanusuru wasiotumia kupata athari inayotokana na moshi wa mtumiaji.

Amesema pamoja na matangazo yanayotolewa na wazalishaji wa sigara kuhusu athari zinazotokana na uvutaji wa sigara na bidhaa zinazotokana na tumbaku, bado matumiza ya bidhaa hizo ni makubwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasiyoambukiza Omar Abdalla amesema vifo vinavyotokana na maradhi yasiyoambukiza vimekuwa vikiongeza kwa kasi ya kutisha .

Amesema kati ya watu kumi wanaofariki hapa Zanzibar, sita hufari kutokana na maradhi yasiyoambukiza na chanzo kikubwa ni kutumia bidhaa zinazotokana na tumbaku na mlo usiokamili.

Kaimu Meneja Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza ameyataja maradhi hayo kuwa ni pamoja na sindikizo la damu, kisukari, saratani ya shingo ya kizazi, tenzi dume, maradhi ya moyo, maradhi ya akili na maradhi ya njia za hewa.

Afisa wa Kitengo cha Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Zuhura Saleh Amour amesema zaidi ya watumiaji tumbaku milioni nane hufariki dunia kila mwaka duniani ambapo milioni 1.2 sio watumiaji lakini wanaathirka kwa kukaa karibu na watumiaji.

Ameweka wazi kuwa ndani ya sigara kuna Nikotini inayosababisha tatizo la koo, mapafu, moyo, chango na kupelekea kudhoofika nguvu za uzazi kwa wanaume na kuaharibika  kwa kizazi kwa upande wa wanawake.

Amesema iwapo jamii itahamasika  kutekeleza kwa ukamilifu kanuni ya tumbaku ya mwaka 2016 maradhi yasiyoambukiza yatapungua kwa kiasi kikubwa na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo  na maradhi hayo.

Loading