NAIBU WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR ATOA TAARIFA YA MAADHIMISHO YA WIKI YA CHANJO KWA WAANDISHI WA HABARI.

Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Mradi Shirikishi Afya ya Uzazi na Mtoto, Kitengo cha Chanjo kuanzia kesho itaungana na nchi nyengine duniani kuadhimisha wiki ya chanjo Afrika itakayoishia tarehe 30 mwezi huu.

Akitoa taarifa ya maadhimisho ya  wiki ya chanjo mbele ya Waandishi wa Habari katika Hospitali ya Mnazimmoja, Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman alisema chanjo hiyo itawahusu watoto walio chini ya miaka miwili na wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao hawajapata ama hawajakamilisha chanjo.

Alisema imethibitika kuwa chanjo ni tiba muafaka wa gharama nafuu katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto na hivyo kupunguza gharama kubwa ambazo familia na taifa lingetumia katika kutibu maradhi yatokkanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Naibu Waziri amewataka wazazi na walezi kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo kwa kuwapeleka watoto wote wenye umri chini ya miaka miwili na wasichana wenye umri wa miaka 14 waliokuwa hawajakamilisha ratiba ili wapate chanjo hiyo ili kujikinga na maradhi.

Aliyataja magonjwa yanayokingwa kwa njia ya chanjo hapa Zanzibar ni pamoja na Kifua kikuu, Dondakoo, Kifaduro, Polio, Surua, Pepopunda, Homa ya ini, Homa ya uti wa mgongo, Kichomi, Kuharisha na Saratani ya Mlango wa kizazi.

Alisema Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika chanjo zilizopita na imeweza kudhibiti ugonjwa wa Ndui, Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda ya watoto wachanga na Surua .

Kutokana na mafanikio hayo alisema Zanzibar imeweza kuwa miongoni mwa nchi zisizo na virusi pori vya Polio vinavyosababisha ulemavu kwa watoto wadogo tokea mwaka 2015 na kuthibitishwa na mashirika ya kimataifa.

Alieleza kuwa mafanikio hayo makubwa yametokana na kufanikiwa kuwapatia chanjo watoto chini ya umri wa miaka miwili nchi nzima kwa zaidi ya asilimia 85.

Hata hivyo alisema bado zipo changamoto za watoto wachache ambao hawajapata chanjo na kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa na kuhatarisha jamii nzima.

Mratibu wa chanjo Yussuf Haji Makame alisema uzinduzi rasmi wa chanjo Kitaifa utafanyika Wilaya ya Kaskazini B katika kituo cha afya Fujoni na Wilaya nyengine zitafanya uzinduzi wa kawaida katika Wilaya zao.

Kauli mbiu ya wiki ya chanjo mwaka huu ni ” Chanjo ni Kinga, kwa pamoja tuwakinge.”

Loading