WAZIRI MAZRUI AKUTANA NA JUMUIYA YA UCHUNGUZI WA VINASABA VYA BINAADAMU TANZANIA

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itashirikiana Jumuiya ya Uchunguzi wa Vinasaba vya Binaadamu ili kugundua maradhi yanayotokana na vinasaba hivyo ili kuyapatia ufumbuzi.

Ameyasema hayo Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui huko Ofisini kwake Mnazi Mmoja, wakati alipotembelewa na Ujumbe kutoka katika Jumuiya ya Vinasaba vya Binaadamu Tanzania, amesema maradhi mengi sana yanasababishwa na vinasaba ikiwemo maradhi ya Urithi.

Amesema maradhi ya vinasaba huanza kuwapata watoto kutokana na jamii kushindwa kuyagundua mapema kwa sababu ya ukosefu wa elimu ya kuyajua na kuyapatia ufumbuzi bila ya kuwaathiri.

Amesema Jumuiya hiyo inafanyakazi sehemu mbali mbali ya kuchunguza vinasaba vya binaadamu, hivyo serikali imejipanga kuimarisha zaidi kitengo cha uchunguzi kilichopo Binguni na kudumisha ushikiano baina yao ili kupata uzoefu.

“Ipo haja ya kushirikiana nao kwani kutaleta maendeleo ya nchi kwa haraka kwani kwenye Afya bora ndio kwenye maendeleo, pia wanauzoefu mkubwa kuhusiana na vinasaba vya binaadamu hivyo watapata kupeana elimu na ujuzi zaidi watakapofanyakazi Zanzibar”, alisema Waziri.

Aidha Waziri Mazrui amesema wamefurahishwa na ujio huo wenye lengo la kuleta mashirikiano na maendeleo katika sekta ya afya nchini.

Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya uchunguzi wa Vinasaba vya Binaadamu Dk. Siana Nkea amesema ameipongeza Wizara ya Afya kwa mashirikiano na mapokezi waliyoyapata na kuonesha utayari wa kufanyakazi ya kuchunguza vinasaba vya binadamu ili kuyagundua na kuyapatia ufumbuzi maradhi hayo.

Amesema Jumuiya hiyo imejipanga kufanya uchunguzi ili kugundua maradhi yanatokanayo na vinasaba vya binaadamu kwa lengo la kuimarisha afya za wananchi pamoja na kutoa elimu kuhusiana na maradhi yatakayogunduliwa.

Dk. Siana alifahamisha kuwa Jumuiya hiyo inatarajia kufungua tawi Zanzibar kwa lengo la kusaidia jamii na kubadilishana ujuzi kuhusiana na maradhi yanayotokana na vinasaba pamoja na kujikinga na maradhi hayo mapema. 

Loading