Mkurugenzi Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar Dkt. Mayasa Salim Ali akizungumza machache na kuwakaribisha wajumbe katika uzinduzi wa mradi wa kuongezea thamani tiba asili, hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mkutano Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar
Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) imetakiwa kuendeleza kufanya utafiti wa dawa za asili ili zitumike kwa usahihi katika kutibu maradhi yasiyoambukiza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uongezaji wa Thamani Tiba za Mimea ya asili katika kutibu maradhi yasiyoambukiza ofisini kwake Mnazi Moja, Mkurugenzi Tiba kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Dk. Amour Suleiman Mohamed, amesema tafiti zinazofanywa zitawasaidia wanajamii kutibu maradhi ya kuambukiza kwa usahihi na kuepuka kubahatisha.
Alisema kuwa, idadi kubwa ya wanajamii hutumia dawa za asili bila kuwa na elimu na kipimo sahihi jambo ambalo husababisha madhara makubwa kwa afya zao.
Alisema ili kuiepusha jamii na madhara hayo, ipo haja ya kutoa elimu juu ya viwango na matumizi sahihi ya dawa hizo ili kuleta matoke chanya ya dawa zinazotumiwa.
“Jamii hutumia dawa asili za mimea bila kiwango, kupitia tafiti hizi zitasaidia kugundua maradhi na kutumia tiba kwa kiwango kinachotakikana ili kuwasaidia wazee wetu majumbani kuweza kutumia dawa kwa usahihi kulingana na majibu sahihi yanayotolewa na tafiti ili kuleta tija” alisema Dk Amour.
Alifahamisha kuwa, dunia ilipokumbwa na janga la Uviko 19 ambayo ni maradhi yanayoambukiza, tiba asili zilisaidia katika kupambana na janga hilo, hivyo ni vyema kuongeza jitihada katika kuzipa thamani dawa hizo za mimea na kuzitumia kama zinavyotumika katika nchini nyengine.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Baraza la Tiba Asili Prof. Hamis Malebo amesema jamii inapaswa kupewa elimu kuhusiana na kuhifadhi na kutunza rasilimali ya mimea dawa, kwani inamchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini.
Vile vile ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar, kwa kuchukua fursa hii muhimu ya kuanzisha mradi huu utakaosaidia kuonesha thamani ya dawa asili zinazotokana na mimea.