KAMATI YA KITAIFA YA KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI ZANZIBAR YAKUTANA KUPANGA MIKAKATI YAKE

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema umefika wakati wa kila mmoja kuwajibika ipasavyo ili kutokomeza vitendo vya udhalilishaji nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Waziri Haroun amesema tatizo la udhalilishaji linaendelea kukemewa vikali na Serikali pamoja na wadau mbalimbali hivyo nguvu ya pamoja inahitajika ili kutokomeza tatizo hilo.

Alisema lengo la kikao hicho kilichoshirikisha wadau mbalimbali wa udhalilishaji ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama ni kukusanya maoni ya wadau ambayo yatasaidia kupanga mikakati madhubuti ya kupambana na udhalilishaji nchini.

Alieleza kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa watoto ni miongoni mwa vitendo viovu ambavyo hudumaza ustawi wa jamii na maendeleo ya watoto wengi nchini.

“Hivi sasa tunataka tumalize kabisa vitendo hivi ili iwe ni historia kwa Zanzibar visiwepo tena vimetutosha watoto wetu bado wanadhalilishwa sasa udhalilishaji basi”, alisema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo alipongeza Serikali kwa kuanzisha mahakama ya udhalilishaji ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza jitihada za kumaliza udhalilishaji nchini.

Loading