Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mh.Hemed Suleiman Abdulla, akisikiliza maelezo kuhusu dawa asili, kutoka kwa mdau wa tiba za asili, nje ya jengo la sanaa Rahaleo, wakati wa hafla ya maadhimisho ya siku ya tiba asili Barani Afrika ,wakwanza kushoto ni Waziri wa Afya ,Ustawi wa Jamii, wazee , Jinsia na Watoto,Mhe. Nassor Ahmed Mazrui
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema dunia inatambua umuhimu wa tiba asili kwa afya ya mwanadamu, hasa katika kipindi cha mripuko wa ugonjwa wa corona
Amesema matumizi sahihi ya tiba za asili, yanamchango mkubwa katika kuimarisha kinga ya mwili na kutibu maradhi mbalimbali ya wanadamu ikiwemo maradhi ya kuambukiza.
Akizungumza na wadau wa tiba asili katika maadhimisho ya siku ya tiba za asili Barani Afrika katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja, amesema Baraza la Tiba Asili Zanzibar, linamchango mkubwa katika kuhakikisha afya za wananchi wa Zanzibar zinaimarika kwa tiba asili.
Alieleza kuwa, wananchi wa Zanzibar ni watumiaji wakubwa wa tiba za asili hasa katika matibabu ya viungo ambayo yamewawezesha kupunguza harakati na muda wa kutafuta huduma hiyo.
Hemed alisema ushirikiano uliopo baina ya wataalamu, watafiti pamoja na serikali unasaidia katika kuhakikisha tiba bora na sahihi inawafikia wananchi wote.
Mhe. Hemed ambae alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo, amelitaka Baraza la Tiba asili kuhakikisha wauzaji wote wa dawa za hizo, wanafuata taratibu na sheria za uuzaji sahihi wa dawa na kuuza katika maeneo yanayoruhusiwa ili kulinda afya ya mtumiaji.
Aliwasisitiza waganga wa asili kutumia utaalamu walionao kwa kuwatibu wagonjwa na sio kuwadhalilisha.
(Sio kila muuzaji wa dawa za asili ana taaluma ya dawa hizo, nawaomba wauzaji wote wa dawa kushirkiana na Baraza la tiba asili, ili kupewa taaluma kwa maendeleo ya sekta ya afya nchini)”, alieleza Mhe. Hemed.
Aliwaasa wananchi kuwa makini katika matumizi dawa za asili, na kufuata malekezo ya wataalamu ili kuepusha madhara yanaweza kujitokeza.
Aidha alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa mchango kubwa wanaoutoa katika kuisaidia sekta ya afya Zanzibar.
Mhe. Hemed alimuagiza Waziri wa Afya kuhakikisha Baraza hilo linapatiwa vitendea kazi vya kutosha, ikiwemo usafiri ili kazi zifanyike kwa ufanisi.
Mapema Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, amesema ipo haja ya kuwepo miundombinu madhubuti ya maabara, ili kufanya uchunguzi wa kina wa dawa za asili kwa lengo la kuepusha madhara kwa watumiaji.
Alisema kuwa, uchunguzi ni miongoni mwa mambo ya msingi, katika afya ya mwanadamu, jambo ambalo litasaidia uaptikanaji wa dawa sahihi kwa wagonjwa na kuepusha tabia ya kubahatisha.
“Ni vyema kuchunguza kwanza na sio kumpa mtu dawa ya asili kwa kubahatisha, ili kutoa matibabu ya uhakika,wananchi wetu lazima tuwaweke salama kiafya”, alisema Waziri Mazrui.
Alilitaka Baraza la tiba asili, kuzidi kutoa ushirikiano kwa vitengo mbalimbali vya afya ili wananchi wapate huduma bora nchini.
Alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kutumia tiba asili kwa usahihi, kwani zinauwezo mkubwa wa kutibu magonjwa ya wanadamu.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Simon Vendelin, amesema asilimia 80 ya waafrika wanatumia tiba asili kwa lengo la kutibu magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
Alisema kuwa, tiba za asili zimetoa mchango mkubwa katika kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi nyingi za afrika.
Alieleza kuwa, ushirikiano wa pamoja unaweza kuiweka Zanzibar katika ramani ya matumizi bora ya tiba za asili.
Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO), linathamini mchango mkubwa wa dawa za asili katika matibabu,, na limeweza kutoa miongozo na fedha kwa ajili ya tafiti mbalimbali nchini.
Alifahamisha kuwa, ni vyema milango ikafunguliwa kwa matabibu na tiba za asili ili dawa hizo ziweze kuthibitishwa kutumiwa.
Siku ya Tiba Asili Barani Afrika huadhimishwa kila ifikapo tarehe 31 Agosti, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni, ni “Mchango wa dawa asili katika kukabiliana na UVIKO-19”.