Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdulla akitoa hotuba ya uzinduzi wa Mafunzo ya Lugha ya alama kwa wafanyakazi wa Bohari kuu ya dawa katika Ukumbi wa Bohari kuu ya Dawa Maruhubi Zanzibar
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdalla amempongeza Mkurugenzi Bohari kuu ya Dawa Zahran Ali Hamad kwa kutekeleza kwa vitendo mafunzo ya lugha ya alama kwa wafanyakazi wake .
Amesema utekelezaji wa mafunzo ya lugha ya alama ni jambo muhimu sana ambalo litasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wenye mahitaji maalum kuweza kufahamiana kwa urahisi pale wanapo taka kupatiwa huduma .
Hayo ameyasema huko katika Ukumbi wa Bohari kuu ya Dawa Maruhubi Zanzibar,.alipokuwa akifungua mafunzo ya lugha ya alama kwa wafanyakazi wa Bohari hiyo.
Alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa Taasisi zote ambazo zinatowa huduma kwa wananchi ili kuweza kujenga uelewa kwa wananchi wenye mahitaji maalumu hasa visiwi kwa kupata huduma kama wengine.
“Sera ya Afya tutoe huduma ya afya bila ya ubaguzi kwa watu wote hata kama wanamahitaji maalumu ya viungo,akili wasioona viziwi na wenye maradhi ya ngozi wote wana haki sawa katika kupata huduma “alisema Katibu huyo .
Katibu huyo amewataka wenye kutoa huduma pamoja na jamii kiujumla ibadilike kwa kujuwa tofauti zilizopo baina yao na kuhakikisha nao wanapatiwa huduma kwa kuzingatia wao hawako katika mfumo wa kawaida kutokana na mapungufu walionayo.
Nae Mkurugenzi Bohari kuu ya Dawa Zahran Ali Hamad aliwataka wafanyakazi hao kuwa makini katika kujifunza mafunzo wa kuweza kujenga uelewa wa kuimarisha mawasiliano wakati wanapotoa huduma kwa wananchi hao ili kuwaondoshea changamoto wanazokumbana nazo .
Aidha alisema ni jambo la kusikitisha kuona watoaji wa huduma za afya ikiwemo madaktari kutoelewana na mgonjwa mwenye mahitaji maalumu jambo ambalo linachangia unyanyasaji na kuhisiwa wanapoteza muda kwa kutofahamiana kwao .
Jambo hilo linachangia kupata unyonge kwa kushindwa kujielezea na kutolewa ukali, kukosa uelewa wa matumizi ya dawa wanazopewa pia kukaa foleni kwa muda mrefu kutokana na kutosikia wakati wakiitwa kupatiwa huduma.

Kwa upande wa Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi Wizara ya Afya Ramadhan Khamis alisema uanzishwaji wa mafunzo hayo muhimu kwa watoa huduma itasaidia kuonyesha njia kwa Taasisi mbali mbali kujifunza ili kusaidia watu wenye mahitaji maalum.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Zanzibar (CHAVIZA) Asha Ali amesema amefurahishwa kwa juhudi ya Wizara ya Afya kuanzisha mafunzo ya alama za vidole kwa watendaji wake ili kuweza kuwarahisishia mawasiliano pale wanahitaji huduma .
Mafunzo hayo ni ya muda mrefu ambayo yamewashirikisha wafanyakazi wote wa bohari kuu ya madawa kwa kila siku nne za masaa mawili ya mwisho katika saa za kazi .