Waziri wa Afya akataza kuomba michango kwa ajili ya Wagonjwa

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo Pichani) kuhusu kukataza kuomba michango kwa ajili ya Wagojwa, huko  Hospitali ya Mnazi Mmoja

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutekeleza sera kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa matibabu bure pamoja na kuwasafirisha  Wagonjwa nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa  Afya Hamad Rashid Mohamed huko Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja katika Wodi ya Wagonjwa wa Ngozi  .

Alisema Serikali haijashindwa kuwahudumia wananchi wake hivyo si vyema kuisambaza picha ya Mgonjwa katika mitandao ya kijamii kwa nia ya kutafuta  michango ya wafadhili kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

“Kuisambaza Picha ya Mgonjwa katika mitandao ya kijamii ni kosa la kumdhalilisha pia kwenda kinyume na Sera ya Serikali”, alisema Waziri Hamad .

Alifahamisha kuwa Serikali inatumia pesa nyingi kununua vifaa tiba ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa matibabu ya uhakika na wale wanaohitaji kusafirishwa nje hupelekwa kwa matibabu zaidi.

Nae Daktari wa Maradhi ya Ngozi katika Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja  Hafidh Sheha Said amekiri kumpokea mtoto Saidi Ali Ayoub mwenye umri wa miaka mitatu kutoka micheweni Pemba mwezi wa nane mwaka 2019  ambae anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi ambao hauwezi kupokea mionzi ya jua .

Alisema Mtoto huyo baada ya kugundulika ana Saratani ya Ngozi katika kichwa chake alisafirishwa na  kupelekwa  Hospitali ya  Muhimbili  kwa kupatiwa matibabu zaidi.

Alifahamisha alirejea kutoka Muhimbili baada ya Wazazi wake kuona tiba anayopatiwa haimpi unafuu bali ni kumuengezea majeraha .

Alieleza ngozi ya watoto kama hawa ambao wanaitwa watoto wa usiku  wakipata mionzi ya jua hupata saratani ya ngozi hivyo hupatiwa mafuta maalum ya kupaka, miwani pamoja na kofia .

Kwa upande wa Baba wa Mtoto Ali Ayoub Hamad aliiomba Serikali kumsaidia kumpatia Matibabu Mtoto wake ili aweze kupoa.

“Nimemzaa mtoto wangu akiwa mzima kufika miezi saba tu akaanza kutoka vidoto vyeusi, vikasambaa kichwani na kutoka vidonda”alisema Baba huyo .

Nae Mkurugenzi wa Alfatah charitable foundation Rashid Salum Mohamed alisema walipigiwa simu kutoka Micheweni Pemba kwamba kuna mtoto ana matatizo anahitaji msaada .

Amesema walifanya juhudi na hadi sasa wameshakusanya zaidi ya shilingi milioni sita kutoka kwa  wafadhili mbali mbali wa ndani na nje ya nchi kwa nia njema ya kutaka kumsaidia mtoto huyo.

Loading