ZANZIBAR KUZINDUA ZOEZI LA KUPIGA DAWA YA MALARIA MAJUMBANI TAREHE 15 MWEZI HUU.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk. Fadhil Abdalla akielezea mauzui ya upiga dawa majumbani katika Mkutano wa Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman na wandishi wa habari uliofanyika Ofisi za malaria Mwanakwerekwe

Wizara ya Afya Zanzibar itazindua zoezi la siku kumi la kupiga dawa ya majumbani ya kuulia viluilui vya Malaria tarehe 13 na kuendelea hadi tarehe 27 mwezi huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya kumaliza Malaria Mwanakwerekwe, Naibu Waziri wa Afya Harusi Saidi Suleiman alisema zoezi hilo litazihusu shehia 76 Unguja na Pemba.

Alisema shehia zitakazopigwa dawa kwa upande wa Unguja ni 67 na Pemba ni shehia 9 ambapo zaidi ya nyumba 41,000 zitahusika katika zoezi hilo.

Alisema baadhi ya shehia katika Wilaya zote za Unguja zitapigwa dawa na pemba ni Wilaya ya Mkoani yenye shehia moja, Wete shehia tano na Micheweni shehia tatu.

Naibu Waziri alisema Wilaya za Unguja zimepatikana na mambukizi ya Malaria kuliko Wilaya za Pemba na ndio sababu ya shehia nyingi za zitapigiwa dawa.

Aliwataka wananchi watakaopigiwa dawa kutoa ushrikiano kwa wapiga dawa wanapofika majumbani mwao na kufanya maandalizi ndani ya nyumba zao na kuweka maji kwa ajili ya kazi hiyo.

Aliwatoa wasi wasi wananchi kuwa vijana watakaofanya kazi hiyo wamepatiwa mafunzo maalumu ya uadilifu na hivyo wasiwe na mashaka nao.

Aliwashauri wananchi watakaopigiwa dawa kuendeleza mikakati ya kujikinga na Malaria kwa kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa na kuacha tabia ya kutumia dawa kabla ya kuthibitishwa kuwa na Malaria.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk. Fadhil Abdalla alisema zoezi la kupiga dawa majumbani ni moja ya mikakati ya inayotumiwa na Wizara hiyo kupambana na Malaria.

Alisema kiwango cha Malaria Zanzibar bado kipo chini ya asilimia moja lakini lengo la Wizara ni kuhakikisha maradhi hayo yanamalizika kabisa.

Mfuatiliaji mwenendo wa maradhi ya Malaria Wahida Shirazi Hassan alisema idadi ya kesi za maradhi ya Malaria ziliongozeka mwaka 2019 ukilinganisha na mwaka 2018 kutoka kesi 5640 hadi kufikia 6760 ambapo wagonjwa watano walifariki.

Loading