MKUTANO WA WATENDAJI WA SERIKALI KUHUSU MASUALA YA WAZEE ZANZIBAR

 Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar (JUWAZA) Aboud Twalib, akizungumzia kuhusu haki na Stahiki mbali mbali zinazowahusu Wazee, katika hafla ya Ufunguzi wa Mkutano Wa Watendaji wa Serikali kuhusu Masuala ya Wazee Zanzibar, uliyofanyika Ukumbi wa Uzazi Salama Hospitali ya Maradhi ya akili Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii , Wazee, Jinsia na Watoto Abeda Rashid Abdalla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inampango wa kuendelea kutowa Vitambulisho kwa Wazee wote na kutumika rasmi katika kupata huduma mbali mbali za kijamii.

Hayo ameyasema wakati akifungua Mkutano wa Watendaji wa Serikali unaohusu Masuala ya Wazee Zanzibar, uliyofanyika Ukumbi wa Uzazi Salama Katika Hospitali ya Maradhi ya akili Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar.

Amesema Vitambulisho hivyo vitawasaidia sana Wazee kwa kupewa kipaumbele katika kupata huduma muhimu kama vile, huduma za Afya, pensheni jamii,Usafiri, Umeme na hata katika Taasisi za Fedha.

Aidha amesema wazee ni watu muhimu katika jamii hivyo ipo haja kwa kila sekta zinazotoa huduma kuwajali kwa kuwapa kipaumbele na kutayarisha sera na mikakati inayohusu upatikanaji wa haki na stahiki zao.

Akiwasilisha mada kuhusu hali ya Wazee Zanzibar  pamoja na masuala ya kisekta yanayowahusu wazee Dr. Salum Rashid Muhammed  amesema ipo haja ya kuwepo uwakilishi wa Wazee Zanzibar katika mikutano mbali mbali ya kitaifa inayofanyika ili kutoa michango  katika sera za maendeleo.

Hata hivyo amesema suala hilo la wawakilishi wa Wazee lina umuhimu mkubwa  kuwepo katika vyombo vya kutoa maamuzi na hasa katika Baraza la wawakilishi na madiwani, halmashauri na mabaraza ya miji kama yanavyoshirikishwa makundi mengine katika kutoa maamuzi.

Aidha amesema lengo la kuwepo uwakilishi wa Wazee litahakikisha upatikanaji wa mahitaji yao katika kuzifikia huduma zote za msingi.

Nae Mratibu wa miradi wa Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar (JUWAZA) Ghanima Othman,amesema malengo ya mkutano huo ni kuandaa mipango maalumu inayowahusu Wazee na kuiboresha kwa kuingiza vipengele vya wazee vilivyopo.

Vile vile amesema Serikali ichukuwe  hatua za kuelimisha jamii juu ya ulinzi na uhifadhi wa Wazee kupitia Wizara  ya elimu kwa kuwasomesha watoto na vijana juu ya umuhimu na namna bora ya kuwatunza na kuwaenzi Wazee.

Sambamba na hayo amesema ipo haja kwa Serikali kuchukua jitihada za ziada katika kuridhia mikataba ya umoja wa Mataifa yanayowahusu wazee na kuhakikisha wanakuwa na uwakilishi katika mikutano ya kimataifa .

Nao wazee walioshiriki katika mkutano huo wameiomba Serikali  kuweka utaratibu maalumu  kwa wazee  kuonana na viongozi  bila kukaa foleni katika kupatiwa huduma.

Loading