MAADHIMISHO YA SIKU YA UNAWAJI MIKONO DUNIANI.

Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii,Wazee Jinsia na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, akisisitiza juu ya umuhimu ya unawaji Mikono, katika hafla ya Maadhimisho ya siku ya Unawaji Mikono Duniani, huko Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul- Wakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto Mhe Nassor Ahmed Mazrui amewataka wananchi kunawa mikono ipasavyo  ili kujikinga na maradhi mbalimbali ya kuambukiza.

Hayo amesema katika maadhimisho ya siku ya unawaji mikono duniani huko katika Ukumbi wa Sheikh Idrisaa Abdulwakil kikwajuni Mjini Unguja.

Alisema unawaji wa mikono ni muhimu sana kwa jamii ili kujikinga na maradhi mbalimbali pamoja na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Aidha Waziri huyo alisema lengo kuu la  maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa jamii juu ya suala zima la unawaji mikono kwa ufanisi na kufuata hatua stahiki katika unawaji.

“Utaratibu maalum wa kuosha mikono unafuata hatua maalum, ambazo ni kutumia maji safi na salama yanayotiririka na sabuni kwa muda usiopungua sekunde ishirini” Alisema Waziri huyo.

Waziri Mazrui amesema tafiti  zinaonesha unawaji mikono kwa maji Safi ni hatua madhubuti za kuzuia magonjwa ya kuambukiza ikiwemo kipindupindu ,kuharisha damu,maambukizi ya macho pamoja na maradhi ya mfumo wa kupumua.

Aidha alisema Wizara yake imetoa elimu katika shehia mbalimbali za Zanzibar kupitia vyombo vya habari, magari ya matangazo, masokoni na shuleni.

Waziri Mazrui amewataka watendaji wa kitengo cha Kinga ya afya kuongeza bidii ya kuandaa vipindi maalum vitakavyosaidia wananchi kujenga tabia ya kunawa mikono.

Nae Mwakilishi kutoka Shirika la kuhudumia watoto duniani UNICEF Marko Musambaz ameiomba wizara ya maji kuhakisha maeneo wanayoishi wananchi yanapata maji safi ili lengo la unawaji mikono lifikiwe.

Mwakilishi huyo alisema shirika la UNICEF liko tayari kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kuhakikisha  huduma za unawaji mikono zinapatikana  katika skuli 121 katika wilaya tano ambazo zinahistoria kubwa za ugonjwa wa kipindupindu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga na elimu ya afya Zanzibar Dkt Ali Nyanga amezitaka  taasisi binafsi kushirikiana na wizara ya afya katika kushajihisha  makundi mbalimbali juu ya umuhimu wa unawaji mikono ili kudhibiti maradhi katika jamii.

Loading