ZANZIBAR YAPATA MUEKEZAJI KIWANDA CHA KUZALISHA DAWA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema iko tayari kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza nchini katika sekta tofauti  ili kukuza  uchumi wa Zanzibar.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Ahmed Nassor Mazrui wakati alipokutana na ugeni wa kampuni ya Afriamco kutoka Emirate ambayo imekusudia kujenga kiwanda cha kuzalisha dawa za binadamu hapa nchini.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya itahakikisha inawapa fursa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo ya Afya ili kuboresha na kuimarisha huduma zinazotolewa.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo utawanufaisha wananchi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na ajira na wanafunzi kupata mafunzo kwa  njia ya vitendo  vya utengenezaji na upatikanaji wa dawa kwa urahisi.

Nae Meneja mkuu wa kampuni ya Afriamco and Mglory Holding Limited Mhandisi Khalid Mohamed Abubakar amesema wanashauku kubwa ya kuwekeza kiwanda cha kuzalisha dawa hapa nchini kwani kutasaidia kupunguza gharama ya uagizaji kutoka nje ya nchi.

Amefahamisha kuwa dawa ambazo zizozalishwa  zitauzwa ndani na nje ya nchi hali ambayo itarahisisha upatikanaji wa dawa kwa bara la Afrika.

Kampuni ya Afriamco ambayo makaazi yake ni Emirate ina  uhusiano wa karibu na Nchi ya China, India na pia imejikita katika nchi 17 katika bara la Afrika.

Loading