NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA ATEMBELEA VITUO VYA KUTOLEA PENSHENI JAMII

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Abeda Rashid Abdalla amesema  Serikali imekusudia kuongeza vituo vya kutolea Pensheni ili kupunguza msongamano kwa wanaofika kupata huduma hiyo.

Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea vituo vilivyomo katika Mkoa wa Mjini Magharibi kuangalia zoezi la utoaji wa huduma hiyo inavyoendelea katika vituo hivyo na kupokea malalamiko kwa wazee.

Amesema Wazee wamekuwa wakipata tabu kutokana na msongamano wa watu wengi katika kituo kimoja jambo ambalo linawafanya wazee kulalamikia kuongezewa vituo vyengine vya utoaji huduma ya Pensheni ili kuondosha usumbufu uliopo.

“Wazee wenyewe ndio wanajua shida wanazopata, wazee wanakuwa ni wengi nafasi ndogo wengine wanakaa  maeneo ya mbali kufika kituoni ni changamoto kubwa kwa wazee hao.” alisema Naibu Katibu.

Aidha Naibu huyo amewataka watendaji wa kitengo cha Pensheni kushirikana na masheha kuandaa mazingira rafiki kwa Wazee katika vituo vitakavyoongezwa kwa ajili ya zoezi hilo.

Nae Mkuu wa kitengo cha Pensheni Jamii Zanzibar Aisha Abass Seif amesema kitengo chake kimeongeza vituo vya utoaji wa huduma hiyo kutoka vituo vitano hadi kufikia saba ambavyo vitaanza kutumika mwezi ujao ili kupunguza msongomano wa wazee kufika katika kituo kimoja kufuata huduma hiyo.

Hata hivyo ameeleza kuwa wameandaa fomu maalum za malalamiko ambazo zitatolewa kwa wananchi kupitia masheha wao na kuzifanyia kazi ili kuona huduma ya Pensheni inawaweka karibu wazee pamoja na watendaji.

Kwa upande wao wazee wamesema wanaridhishwa na utoaji wa huduma hiyo japo kuwa haikidhi mahitaji ya kila kitu hivyo wameiomba serikali kuwaongezea Pensheni hiyo.

Mapema Bi Abeda alitembelea kituo cha Wazee Welezo na kuwapatia vitambulisho maalum vitakavyosaidia kuwatambulisha pindi wakiwepo mazingira ya nje ya kituo hicho kuweza kupata msaada kwa urahisi. 

Loading