Wasafiri kufanya vipimo vya Covid kwa njia ya mtandao Zanzibar

Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia, Wazee na Watoto itaanzisha zoezi  la vipimo vya Covid kwa wasafiri wanaoingia na kutoka Zanzibar kwa njia ya Mtandao kuanzia tarehe tisa mwezi huu.

Uwamuzi huo umeandaliwa ili kukabiliana na vyeti feki na kuondosha usumbufu na msongamano wa wasafiri kwenye vituo vinavyoendesha zoezi hilo Mazizini na Lumumba kwa Unguja na kituo kimoja kilichopo Pemba.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Mnazimmoja, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Omar Dadi Shajak alisema Wizara inajiandaa kuanzisha vituo vyengine katika maeneo yenye Hoteli nyingi ili kuongeza ufanisi.

Dkt. Shajak alisema bei ya kipimo cha Covid kimaongezeka kufikia dola 80 kwa watu wote kutokana kuongezeka gharama ya kununulia mashine za kupimia maradhi  hayo.

Hata hivyo alisema wananchi wa Zanzibar hawana haja ya kulalamika kupanda bei kipimo cha Covid kwa sababu sio suala la matibabu bali ni matakwa ya mashirika ya ndege kwa wasafiri kulazimisha wawe na vyeti vya maradhi hayo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya aliongeza kuwa kutoa bure kipimo cha Covid, kama zinavyotolewa huduma nyengine za afya, ama kupunguza bei ni kuwaongezea mzigo wa maisha wananchi wengine bila ya sababu za msingi.

Wakati huo huo Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia, Wazee na Watoto imetiliana saini mkataba wa ushirikiano wa miaka mitatu na Hospitali ya SIMS ya India.

Kupitia mkataba huo uliotiwa saini na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Omara Dadi Shajak na Meneja wa nchi za nje wa SIMS, Zanzibar itafaidika kwa kuwapeleka wagonjwa India watakaoshindwa kupata matibabu Hospitali ya Mnazimmoja na Hospitali za rufaa za Tanzania Bara .

Dkt. Shajak alisema maeneo mengine yaliyomo ndani ya mkataba huo ni kupatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi madaktari wa Zanzibar nchini India na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya SIMS kuandaa kambi za uchunguzi wa maradhi mbali mbali kwa gharama zao na Serikali kuhudumia matibabu.

Loading