ZANZIBAR YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema jumla ya watoto 508 Unguja na Pemba wanakabiliwa na changaamoto mbalimbali zikiwemo ukiukwaji wa haki zao pamoja na kunyimwa matunzo, mvutano wa malezi kwa wazazi.

Hayo ameyasema huko Wizara ya Afya wakati akizungumza na Waandishi wa habari kufuatia siku ya Mtoto wa Afrika, Unguja ni watoto 251 na Pemba ni257 .

Aidha amesema matukio mengine ni 347  ambayo yanahusiana na watoto kunyimwa matunzo, Unguja 139 na Pemba 208 na 161 yanatokana na mvutano  wa malezi.

Vilevile Mhe. Mazrui amesema siku ya Mtoto wa Afrika ina umuhimu mkubwa katika kupima utekelezaji wa haki za watoto na kupendekeza hatua madhubuti zichukuliwe kwa nia ya kuimarisha huduma zinazolenga watoto na watendaji.

Amesema siku ya Mtoto wa Afrika inatoa msukumo wa kuzidisha ushirikiano baina ya wazazi na walezi sekta zinazohudumia mama na watoto pamoja na wadau wa maendeleo katika kusimamia na kutekeleza sheria.

Aidha amesema misingi mikuu ya kuzingatia uimarishaji na utekelezaji wa haki za watoto ni kuishi, kulindwa kuendelezwa kushirikishwa inahitaji kuwekwa mazingira rafiki na miundo mbinu inayokwenda sambamba na hali ya utamaduni.

Hata hivyo Mhe. Mazrui ameitaka jamii, mashirika na taasisi mbalimbali ziendelee na uwekaji wa mikakati itakayoweza kufanikisha upatikanaji wa haki za watoto na kuimarisha familia kwa kuwadhibiti watoto ili kuwaepusha na maradhi ya COVID 19 pamoja na  vitendo vya ukatili na udhalilishaji.

Vilevile ametoa wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kuwalinda dhidi ya watu wenye nia mbaya ambapo hatua hiyo itasaidia kuashiria vitendo vyovyote vya ukatili na udhalilishaji na kujenga jamii bora.

Siku ya Mtoto wa Afrika Duniani huadhimishwa kila ifikapo June 16 na Ujumbe wa Mwaka huu Utekelezaji Ajenda 2040 inayolinda haki za Watoto.

Loading