UWASILISHAJI WA RIPOTI YA UTAFITI WIZARA YA AFYA, USTAWI WA JAMII, WAZEE, JINSIA NA WATOTO

Daktari Bingwa wa Maradhi ya Akinamama na uzazi katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Dkt, Umulkurthum Omar amesema utafiti umeonyesha maradhi ya Presha ni sababu kubwa ya vifo kwa wazazi ambayo hutokezea wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.

Hayo aliyasema katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja wakati akisoma ripoti ya utafiti huo kwa wajumbe mbali mbali waliowakilisha vituo vyao .

Alisema kuwa tatizo la presha kubwa  kwa akinamama wajawazito ni hatari kwani huchangia kupata  kifafa cha mimba, kupoteza damu nyingi na hata kupata kilema cha kudumu kama asipopata matibabu ya haraka  .

Alifahamisha kuwa katika mwaka 2020 asilimia 28 ya vifo vya mama  wajawazito vilichangiwa na maradhi ya  presha na katika kipindi cha nyuma hali haikupishana jambo ambalo linahitaji  kupatiwa mipango ya muda mrefu ya kuimarisha huduma  kwa kiwango ambacho kitawasaidia akinamama hao

Aidha alisema bado kunahitajika elimu ya kutosha katika jamii kwa kupewa uelewa wa kuhudhuria vituo vya afya mapema wakati wa ujauzito jambo ambalo litaonyesha mwenendo wa afya na kupatiwa  huduma za matibabu pamoja na kupewa ushauri nasaha .

Nae Mtoa Mada  Dkt Omar Mwalimu amesema matatizo ya akinamama wajawazito ni mengi hivyo ipo haja ya  kuyachukulia hatua ikiwemo imani potofu katika jamii ambayo inachangia ucheleweshwaji wa mgonjwa kupatiwa huduma ya haraka .

Aliwataka wahudumu wanaoshughulikia akinamama wajawazito kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ipasavyo ili kuwapa maelekezo na ushauri utakaoweza kuwasaidia akinamama hao .

Akitoa wito kwa wahudumu wa afya alisema kuwa iko haja kukaaa karibu zaidi na jamii ili kuwapa muongozo wa kiafya  ambao utasaidia kuimarisha afya ya mama mjamzito na mtoto kwa kuepukana na matatizo .

Loading