UWASILISHAJI WA MATOKE YA UTAFITI KUHUSU SHINDIKIZO LA DAMU KWA MAMA WAJAWAZITO

Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto imeitaka  jamii kuwa na utamaduni wa kuchunguza  afya mara kwa mara itasaidia  kugundulikana mapema kwa maradhi  ikiwemo maradhi yasioambukiza .

Ushauri huo umetolewa na Daktari Bingwa wa Maradhi ya Akinamama na uzazi katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Dkt, Umulkurthum Omar wakati akisoma matokeo  ya utafiti kwa wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na maafisa elimu wa wilaya katika ukumbi wa Hospitali ya Kidongo Chekundu.

Alisema tafiti zinaonyesha kuwa maradhi yasioambukiza ikiwemo presha, sukari na kensa  ni tatizo sugu duniani  kote, jambo linalopelekea ongezeko la vifo siku hadi siku hasa kwa mama wajawazito.

Aidha alisema maradhi  yasioambukiza hasa presha huwaathiri zaidi  akinamama wajawazito hivyo aliwataka akinamama  wajawazito kuhudhuria klinik mapema ili kuchunguzwa afya zao na kupatiwa huduma za haraka .

“Iwapo wajawazito watahudhuria kliniki kwa wakati itasaidia kujulikana hali zao za kiafya mapema ili kupatiwa msaada wa haraka na kupata ushauri wa kuilea mimba yake ”alifhamisha Daktari  Ummi.

Alisema kuwa kati ya akinamama wajawazito 100 wanaopata huduma katika hospitali kuu ya Mnazimmoja  25 hugundulika na  Presha ambayo inasababishwa na msongo wa mawazo unaotokana na matatizo mbalimbali ya kimaisha.

Alieleza kuwa presha kubwa kwamama mjamzito hupelekea kifafa cha mimba ambacho husababisha kifo kwa mama au ulemavu wakudumu ikiwemo matatizo ya moyo na kufeli kwa figo

Alisema tafiti zilizofanywa za miaka mitatu kwa akinamama wajawazito waliojifungulia hospitali ya rufaa mnazimmoja zimeonyesha kuwa mnamo mwaka 2018  akinamama waliojifungua ni 11,734  waliopata presha kubwa yenye dalili ya kupata kifafa cha mimba ni 123  na waliopata kifafa ni  44 sawa na asilimia 1.14.

Katika mwaka 2019 akinamama  waliojifungua ni 14,832  waliopata presha kubwa ambayo inapelekea kupata kifafa ni 348 na waliopata kifafa ni 54 sawa na asilimia 2.75.

Vile vile utafitiwa mwaka 2020 jumla ya akinamama wajawazito waliojifungua hospitalini hapo ni 13,529   waliopata presha kubwa ambayo inapelekea kupata kifafa cha mimba   ni 331 na waliopata kifafa ni 44 sawa na asilimia 3.54.

Daktari Ummu alifahamisha kuwa  utafiti uliofanywa ulionyesha  uchelewaji wa akinamama wajawazito kliniki, ukosefu wa elimu na ushauri nasaha huchangia kwa kiasi kikubwa kukosekana kupatiwa matibabu kwa haraka .

Aidha alisema katika  mwaka 2020  asilimia 28 ya vifo vya mama  wajawazito vilichangiwa na sababu ya  presha.

Nae Mkufunzi Dkt Omar Mwalimu amesema katika utafiti huo umeonyesha bado zipo imani potofu katika jamii zetu zinazochangia uzoroteshaji wa huduma kwa wajawazito jambo ambalo husababisha kifo.

Akitoa wito kwa wahudumu wa afya alisema kuwa iko haja kukaaa karibu zaidi na jamii ili kuwapa muongozo wa kiafya  ambao utasaidia kuimarisha afya ya mama mjamzito na mtoto .

Utafiti huo  kuhusu shindikizo la damu kwa mama wajawazito ulifanywa na kitengo cha maradhi yasioambukizwa ukijumuisha mikoa mitano ya Zanzibar .

Loading