Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar imewataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi juu ya wimbi jipya la viashiria vya maradhi ya Corona lilizozuka Duniani.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya kuzuka kwa wimbi hilo Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Mh, Nassor Ahmed Mazrui katika Ukumbi wa Wizara hiyo Mnazimmoja amesema tayari nchi jirani ikiwemo Uganda zimekubwa na wimbi hilo.
Amesema kufuatia hali hiyo wananchi hawana budi kuchukua tahadhari za kujikinga zaidi hasa katika mikusanyiko ya watu ili kujikinga na maradhi hayo.
Waziri Mazrui amefahamisha kuwa Wizara imepata taarifa ya kuzuka kwa wimbi hilo kutoka nchi ya Uganda ambayo ina uhusiano mkubwa na Tanzania hasa ukizingatia kuwa bado haijafunga mipaka yake kutokana na shughuli za muingiliano wa kibiashara.
Alifafanuwa kuwa tahadhari hiyo imetolewa mara baada ya kupata taarifa ya kufungwa kwa Vyuo na Maskuli nchini Uganda kutokana na uwepo wa maradhi hayo yaliyoshika kasi na kuenea kwa haraka.
Akieleza mikakati ya kujikinga na maradhi hayo Serekali imeamua kuongeza juhudi zaidi kwa kuwataka wageni wote wanaoingia Nchini kuja na vyeti vyao walivyopimia maradhi ya corona kwa udhibitisho zaidi.
Pia ameeleza kuwa elimu ya Afya ya jamii itatolewa zaidi kuhusu kujikinga na maradhi hayo kupitia vyombo vya habari na Maskulini ili kudhibiti mapema maambukizi yasitokee.
Amesisitiza kuwa vituo vyote vya afya Unguja na Pemba kuwe na utaratibu maalum iwapo atatokea mgonjwa ana dalili za maradhi hayo kufanyiwa vipimo vya haraka na kuacha kukaribiana baina ya mtu na mtu ili kuepusha maambukizi.
“Tunachukua tahadhari ya kujikinga zaidi kwa kufanya yale yote yanayotakiwa kufanya kwa ajili ya kujikinga ikiwemo kuvaa barakoa,kunawa mikono kila wakati kwa kutumia maji na sabuni na endapo atatokea mtu anajihisi anadalili na anahitaji kulazwa basi atupigie kupiga simu namba hizi 0772502513 kwa hatua zaidi,”alisema Waziri huyo
Aidha amesema kuwa Serekali inafanya jitihada ili Wazanzibar waweze kupata chanjo kwa wanaotaka ambayo itathibitishwa na kamati ya uchunguzi iliyoweka na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mh Samia Suluhu Hassan na kwa kuanzia itaanza kwa wafanyakazi wa vituo vya Afya ,Vituo vya Usafirishaji Uwanja wa ndege na Bandarini.
Hata hivyo amewatoa wasiwasi wananchi kuwa kwa hapa Zanzibar hakuna taarifa ya mtu aliegundulika kuwa na maradhi hayo na endapo atagundulika taarifa itatolewa kama wanavyofanya Nchi nyengine.