MAADHIMISHO YA SIKU YA USIKIVU DUNIANI YAADHIMISHWA ZANZIBAR

Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Harusi Said Suleiman akiwahutubia wananchi walioshiriki maadhimisho ya siku ya Usikivu Duniani katika Viwanja vya Mapinduzi Michezani Mjini Unguja

Jamii nchini imetakiwa kwenda hosptali mapema kutafuta matibabu ya Maskio pale tu wanapoanza kuhisi tatizo badala ya kusubiri hali ya afya kuwa mbaya.

Kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutibu tatizo la usikivu ambalo linatibika nchini.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman ametoa wito huo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya usikivu duniani kilichofanyika Kisonge mjini Zanzibar.

Amewaasa wazazi kuacha tabia ya kuwasafisha Masikio watoto wao wachanga kwa kutumika Vijiti vya kusafisha masikio ambavyo husababisha madhara ya usikivu kwa watoto hao.

“kwa mujibu wa madaktari imeonekana pia Wazazi wengi husababisha tatizo la usikivu kwa watoto wao kupitia kuwasafisha masikio kwa Vijiti vya kusafishia masikio. Vile vijiti imeonekana vinaleta madhara tujiepusheni navyo” alinasihi Naibu Waziri.

Dkt. Mkuu wa Pua,Koo na Masikio Naufal Kassim, akitoa historia fupi kuhusiana na maradhi ya Usikivu katika maadhimisho yaliofanyika Viwanja vya Mapinduzi Michezani Mjini Unguja

Amesema kwa sasa imebainika Spika za kuweka masikioni (Earphone na Headphone)na makelele ya Muziki huchangia pakubwa katika matatizo ya usikivu hivyo ni vyema watu wakajiepusha nazo.

“Imebainika kuwa earphone na headphone sambamba na muziki wa makelele, Disko na marusha roho zinachangia sana kuharibu masikio yetu, tuweni makini navyo” alitahadharisha Naibu Waziri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani WHO ofisi ya Zanzibar Dkt. Adrymichel Girmay amesema tatizo la usikivu bado ni kubwa na Ofisi yake ina jukumu la kusaidia kuhakikisha tatizo hilo linapungua.

Amesema WHO itashirikiana vyema na Wizara ya Afya katika kuongeza uelewa wa wananchi juu ya kujikinga na tatizo la usikivu.

Amefahamisha kuwa tatizo hilo linaathiri kwa asilimia tano ya watu wote duniani hivyo juhudi zinapaswa kuchukuliwa ili kulipunguza.

Kwa upande wake Daktari dhamana wa Maskio Hospital ya Mnazi mmoja Dkt. Noufil Mohamed amesema kwa nchi zilizoendelea ikiwemo nchi za Ulaya hakuna tena tatizo la usikivu.

Amefahamisha kuwa hali hiyo inatokana na utaratibu mzuri unaofuatwa katika nchi hizo wa kuwapatia watoto vipimo na tiba mzuri mapema.

“Ulaya hakuna tena Viziwi toka mapema watu hupata tiba mapema ikiwemo kupatiwa vifaa vya kusaidia kusikia” alisema Dkt. Nofil.

Balozi Mdogo wa China Zanzibar Mr. Xie Xiaowu akizungumza machache kuhusu namna ya Nchi yake inavyojitahidi kutoa Mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia sekta ya Afya

Awali akitoa salamu kutoka Shirika la Misaada la China Balozi mdogo wa nchi hiyo ofisi ya Zanzibar Xie Xiaowu amesema Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar hasa katika sekta ya Afya ikiwemo nafasi za masomo kwa wataalamu wake.

Amesema kufanya hivyo kutaiwezesha Serikali ya Zanzibar kuweza kukabiliana vyema na mahitaji ya afya ya wananchi wake.

Katika maadhimisho hayo wananchi pia walipata nafasi ya kuchunguzwa afya zao hasa maskio na kupatiwa Tiba kutoka kwa wataalam wa Wizara ya afya wakishirikiana na wenzao kutoka nchini China.

Loading