UTIAJI WA SAINI WA UJENZI WA HOSPITALI KUMI ZA WILAYA UNGUJA NA PEMBA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia, na Watoto Fatma Mrisho akisaini mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa hospital ya Wilaya ambayo itajengwa Makunduchi  na Mkandarasi Ali Nassor wa kampuni ya ujenzi ya Quality building, hafla iliyofanyika  Wizara ya Afya Mnazi mmoja Mjini Unguja

Katibu Mkuu Wazara wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Fatma Mrisho  ametia saini mikataba  ya makubaliano ya  ujenzi wa Hospitali za Wilaya zinazotarajiwa kujengwa hivi  karibuni katika Wilaya mbalimbali za Unguja na Pemba.

Zoezi hilo la utiaji saini lilifanyika katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar, na kuhusisha kampuni mbalimbali ikiwemo kampuni ya CRJE ya nchini China, kampuni ya WCEC limited, Quality Building Contractors pamoja na kampuni ya Rans Building Contractors.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Fatma Mrisho alisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na nia ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi  ya kutaka kujenga Hospitali kumi za Wilaya  Zanzibar  ili kuboresha huduma za afya nchini.  

Alisema kuwa, ujenzi huo unatarajiwa kuanza hivi karibuni na kukamilika ndani ya muda mfupi  ili wananchi waweze kupatiwa huduma bora za afya katika hospitali hizo kila Wilaya.

“Kwa upande wetu kama Wizara tunajipanga katika kuhakikisha mara tu baada ya kukamilika ujenzi huo vifaa vyote ikiwemo gari za kubebea wagonjwa zinapatikana  pamoja na wafanya kazi wote wanaohitajika wanapatikana ili huduma zitolewe kwa haraka na kwa uafanisi mkubwa”: alisema Katibu.

Aidha alisema ujenzi wa hospitali hizo ni miongoni mwa jitihada za serikali katika kuboresha huduma za afya nchini, na ni njia moja wapo ya kuondoa tatizo la msongamano wa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.

 Mikataba hiyo ilihusisha ujenzi wa hospitali mbalimbali ikiwemo hospitali ya Chumbuni, Magogoni, Mbuzini, Pangatupu, na Makunduchi.

Loading