WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR AFANYA UZINDUZI WA KAMPENI YA UGAWAJI VYANDARUA KITAIFA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na Wafadhili mbalimbali katika kupiga vita dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini.

Hayo aliyasema Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui,  wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Ugawaji wa Vyandaruwa uliofanyika Kitaifa Katika Uwanja wa Demokrasia , Kibandamaiti .

Alisema kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali katika  kudhibiti ugonjwa wa malaria, maambukizi yamepungua hadi kufikia kiwango cha  asilimia moja kwa muda wa miaka kumi hivi sasa .

Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada mbali mbali zilizochukuliwa na Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na watoto ikiwemo kutoa taaluma juu ya kujikinga na malaria kwa wanajamii.

Waziri Mazrui aliwataka wananchi kuzidisha mashirikiano katika mapambano dhidi ya malaria, kwa kutumia vyandaruwa vilivyotiwa dawa, na kusafisha mazingira ili kuondokana na mazalio ya mbu.

Alifafanuwa kuwa, zoezi la ugawaji wa vyandarua vilivyotiwa dawa, litaanza tarehe 24 Julai, 2021 kwa baadhi ya Shehia za Unguja na Pemba.

“Zoezi hilo litajumuisha shehia 335 za Zanzibar,jumla ya wananchi 1,373,872 watanufaika kwa kupata vyandarua vilivyotiwa dawa”, alisema Waziri Mazrui.

Alifahamisha kuwa kinga dhidi ya malaria inahitajika ili kupunguza ongezeko la wagonjwa hao, hivyo aliwataka wananchi kufunika makaro,  michirizi ya maji sehemu za ujenzi, kufunika mahodhi ya maji safi majumbani pamoja na misikitini .

Alieleza kuwa ni vyema wananchi wakatoa ushirikiano  katika zoezi la upigaji dawa muda ukifika, pamoja na kufika mapema katika vituo vya afya iwapo mtu atapata dalili za homa ya malaria kwa  kuumwa na viungo vya mwili.

Vile vile aliwaomba wananchi kufika vituo vya afya ili kuchunguza vimelea vya malaria kabla ya kutumia dawa pamoja na kukamilisha dozi ya dawa za kutibu malaria kwa wale waliopata ugonjwa wa huo .

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Simai Msaraka, amewaomba wananchi kushirikiana katika kupiga vita  malaria ili kulinda afya zao ili kujenga taifa bora.

”Zanzibar kwetu tuhakikishe tunapambana na malaria na kuyaondoa kabisa na kuwa na afya bora ya kujenga taifa letu “alisema Mkuu wa Wilaya ya Mjini.

Nae Kaimu Meneja Programu ya Kumaliza Malaria, Dk. Faiza Bwanakheri Abass alitoa wito kwa wananchi kuweka mikakati ya kupambana na malaria, kwa kuvitumia vyandarua  vilivyotiwa dawa ipasavyo ili kumaliza malaria Zanzibar.

Alisema kwa kipindi cha Julai 2019 mpaka Juni 2020 jumla ya wagonjwa 13,208 waliripotiwa, kati ya hao asilimia 27 walihusishwa na kusafiri nje ya Zanzibar, na vifo 20 vilisababishwa na ugonjwa huo.

Wakati huo huo Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alizindua na kuchanjwa chanjo COVID 19 aina ya Cinovac kutoka nchini China .

Amesema kuwa Chanjo hiyo ni hiyari ambayo iko salama na haina madhara kwa jamii  imethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) .

Waziri Mazrui alieleza kuwa Chanjo hiyo inatolewa bila ya malipo kwa anaetaka kinga hiyo.

Loading