WAANDISHI WA HABARI WAPATIWA MAFUNZO KUHUSU CHANJO YA KIPINDUPINDU DOZI YA PILI

Msimamizi wa Chanjo ya Kipindupindu Unguja Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla amesema chanjo ya kipindupindu haina mahusiano na chanjo ya corona 19 na wala haina madhara yoyote kwa binadamu.

Hayo ameyasema huko Ukumbi wa Sanaa Rahaleo  wakati alipokuwa akitoa  mafunzo kwa Waandishi wa Habari kuhusu Umuhimu wa kumaliza Dozi ya Pili ya chanjo hiyo

Amesema chanjo  ya kipindupindu hutolewa kwa njia ya kumiminika tofauti na chanjo ya covid 19 ambayo hutolewa kwa njia ya sindano na huingia moja kwa moja kwenye damu.

Ameeleza kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya chanjo hizo ni kutokomeza kabisa majanga hayo nchini hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.

Aidha Dk. Fadhili amewasihi  wananchi kuondokana na uvumi unatolewa na baadhi ya wananchi ambao wana lengo la kurejesha nyuma maendeleo ya Zanzibar.

Akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Chanjo ya kipindupindu Dozi ya Pili  Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya Halima Khamis amesema atakaemaliza dozi kamili ya chanjo ya kipindupindu ataepukana na ugonjwa huo kwa muda mrefu.

Bi Halima amewataka wananchi kuendelea kufuata kanuni za kujikinga na maradhi ya kipindupindu ili kuhakikisha Zanzibar inatokomeza kabisa ugonjwa huo.

Hata hivyo  amewasisitiza  waandishi wa habari  kuihamasisha  jamii kujitokeza kwa wingi katika awamu ya pili ya chanjo ya kipindupindu ambayo imeanza tarehe 8/08/2021 mpaka 11/08/2021.

Loading