KATIBU MKUU MPYA AKABIDHIWA RASMI OFISI

Waziri wa Afya ,Ustawi wa Jamii, Wazee ,Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui amewataka watendaji wa wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya awamu ya nane.

Hayo aliyasema katika hafla ya makabidhiano ya ofisi ya Katibu Mkuu yaliyofanyika Wizarani  hapo mara baada ya kuapishwa kwa Katibu Mkuu mpya waWizara hiyo

Alisema watendaji wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii, ili sekta ya afya iweze kuimarika nchini.

Mazrui amewataka watendaji kujitathmini ili waweze kuimarisha utendaji wa kazi, pamoja na  kurekebisha kasoro zinazojitokeza kwa lengo la kuleta ufanisi kazini.

Aidha, amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kumpa ushirikiano Katibu Mkuu mpya ili aweze kutumia uwezo wake katika kuleta mafanikio ya wizara hiyo .

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ofisi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii, Wazee ,Jinsia na Watoto Dkt Fatma Mrisho amesema atahakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya katika maeneo yote ya mijini na vijijini.

Amewataka wafanyakazi kubuni mikakati itakayosaidia katika kuleta maendeleo ya sekta ya afya.

Nae aliyekuwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Omar Dadi Shajak amemtaka katibu huyo kuhakikisha huduma za afya zinapatikana ikiwemo upungufu wa vifaa tiba ,madaktari bingwa katika hospitali za rufaa na wilaya.

Aidha  amewashukuru wafanyakazi wa wizara hiyo kwa kipindi chote walichokuwa pamoja na kuwataka wampe Ushirikiano  katibu huyo kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora.

Loading