WAZIRI WA AFYA ASAINI MSAADA KUTOKA IOM

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jami,i Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui (katikati) akisaini  hati ya makabidhiano ya msaada wa vifaa  mbalimbali  kwa ajili ya matumizi katika nyumba salama, wapili kutoka kushota ni Mwakilishi Mkaazi  kutoka Shirika la  Umoja wa Mataifa la Uhamiaji  IOM Nchini Tanzania Dk.  Qassim Sufi nae akisaini hati hiyo, makabidhiano hayo yalifanyika Ukumbi wa nyumba za kuhifadhia  Wazee Welezo.

Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui  amewataka wazazi na walezi kushirikiana na Serikali katika mapambano ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto  nchini .

Hayo ameyasema katika Nyumba ya kulelea Wazee, Welezo wakati wa makabidhiano ya vifaa vya matumizi mbali mbali kwa ajili ya nyumba salama ya kuhifadhia wahanga wa udhalilishaji kutoka kwa Muakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji Nchini Tanzania  (IOM) Dr Qasim Sufi .

Amesema vitendo vya udhalilishaji ni janga la kitaifa hivyo iko haja jamii kiujumla kushirikiana kwa pamoja na Serikali ili kuhakikisha vitendo hivyo vinaondoka katika jamii .

Aidha ameitaka jamii kutokuwa na muhali wa kuwaficha wahalifu wa vitendo hivyo kufanya hivyo kutasaidia mapambano ya vita dhidi ya udhalilishaji .

“Ni wajibu wetu kushirikiana kwa pamoja kuunga mkono  mapambano ya vita dhidi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto tuacheni muhali, tuwe mstari wa mbele kwa kutoa ushahidi wa ukweli .“alisema Waziri .

Nae Muakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji Nchini Tanzania  (IOM) Dr Qasim Sufi  amesema iko haja kusaidia nyumba salama hapa Zanzibar kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji .

Amesema tatizo hilo ni la kidunia ambalo limekuwa likiwaathiri hususan wanawake na watoto ambao wameonyesha kuathirika zaidi duniani kote.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee, Abdalla Saleh Omar amesema nyumba salama inapokea watoto waliofikwa na kadhia mbali mbali ikiwemo udhalilishaji wa kingono kama  kubakwa, kulawitiwa pamoja na kupigwa kupitiliza .

Pia amesema usafirishaji haramu wa  wahanga ambao hutumika kwa  kufanyakazi za majumbani wakiwa katika umri mdogo hupatia hifadhi ya muda watoto hao, ambapo kwa kipindi cha mwezi wa Agosti hadi Oktoba mwaka huu wahanga walipokelewa 22 katika nyumba salama  kwa hifadhi ya muda.

Hata hivyo alisema wahanga hao wa kike ni 19 na wa kiume ni 3 wengine hupelekwa  katika nyumba salama kwa shaka ya kudhurika ikiwa wazazi wakishtukiwa kuwa watumiaji wa madawa ya kulevya pamoja na watoto waliokosa jamaa hapa Zanzibar .

Loading