Daktari Bingwa wa Maradhi ya Akinamama na uzazi katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Dkt, Umulkurthum Omar amesema utafiti umeonyesha maradhi ya Presha ni sababu kubwa ya vifo kwa wazazi ambayo hutokezea wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.
Hayo aliyasema katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja wakati akisoma ripoti ya utafiti huo kwa wajumbe mbali mbali waliowakilisha vituo vyao .
Alisema kuwa tatizo la presha kubwa kwa akinamama wajawazito ni hatari kwani huchangia kupata kifafa cha mimba, kupoteza damu nyingi na hata kupata kilema cha kudumu kama asipopata matibabu ya haraka .
Alifahamisha kuwa katika mwaka 2020 asilimia 28 ya vifo vya mama wajawazito vilichangiwa na maradhi ya presha na katika kipindi cha nyuma hali haikupishana jambo ambalo linahitaji kupatiwa mipango ya muda mrefu ya kuimarisha huduma kwa kiwango ambacho kitawasaidia akinamama hao
Aidha alisema bado kunahitajika elimu ya kutosha katika jamii kwa kupewa uelewa wa kuhudhuria vituo vya afya mapema wakati wa ujauzito jambo ambalo litaonyesha mwenendo wa afya na kupatiwa huduma za matibabu pamoja na kupewa ushauri nasaha .
Nae Mtoa Mada Dkt Omar Mwalimu amesema matatizo ya akinamama wajawazito ni mengi hivyo ipo haja ya kuyachukulia hatua ikiwemo imani potofu katika jamii ambayo inachangia ucheleweshwaji wa mgonjwa kupatiwa huduma ya haraka .
Aliwataka wahudumu wanaoshughulikia akinamama wajawazito kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ipasavyo ili kuwapa maelekezo na ushauri utakaoweza kuwasaidia akinamama hao .
Akitoa wito kwa wahudumu wa afya alisema kuwa iko haja kukaaa karibu zaidi na jamii ili kuwapa muongozo wa kiafya ambao utasaidia kuimarisha afya ya mama mjamzito na mtoto kwa kuepukana na matatizo .