WAZIRI WA AFYA AFUNGUA KONGAMANO LA KUTATHIMINI KAZI ZA WAKUNGA NA WAUGUZI ZANZIBAR

Wauguzi na Wakunga Nchini wametakiwa kufata maadili na sheria za kazi katika kutekeleza majukumu yao ili kutoa huduma bora kwa  wazazi na wananchi wa Zanzibar.

Akizungumza mbele ya wauguzi na wakunga katika kongamano la kutathmini kazi za Uuguzi na Ukunga Zanzibar, lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil,  Kikwajuni Mjini Unguja, Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto,  Nassor Ahmed Mazrui amesema umefika wakati wa kutathmini namna ya kuengeza hadhi ya wakunga na wauguzi Nchini.

Waziri Mazrui ambae alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, amesema ni vyema kwa kila muuguzi na mkunga kutathmini utendaji wake ili kwenda sambamba na maadili ya kazi yake na mafunzo aliyopewa chuoni.

Alieleza kuwa, ni lazima kila mwanajamii apewe huduma zinazostahiki anapofika hospitali, na kuacha kumtendea kinyume na maadili ili kuepusha malalamiko kwa wananchi.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa,  malalamiko yamepungua kwa asilimia kubwa na huduma zimeboreka, lakini lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kutoa huduma bora  za afya, na kumaliza kabisa malalamiko ya wananchi.

“ Wananchi wetu wanapenda kuona mabadiliko katika utoaji wa huduma za afya, sisi kama Wizara tunajitahidi kuchukua jitihada mbalimbali ili huduma bora zitolewe kwa wananchi Mjini na Vijijini, tupo tayari kupokea malalamiko, maoni na ushauri ili tuweze kupanga mikakati mizuri”. alisema Waziri huyo.

Aidha Waziri Mazrui alitumia fursa hiyo kuwaasa wahudumu na wakunga wanawake, kutumia lugha nzuri na  kuacha kutumia lugha zisizofaa kwa akina mama wajawazito wanaofika hospitalini kujifungua.

Alisisitiza kuwa, ni lazima tathmini ifanyike juu ya njia bora ya kuokoa maisha ya watoto na sio kuwasababishia kifo au ulemavu.

“Muuguzi anatakiwa kufanya kazi kwa moyo wa huruma na upendo, na anatakiwa aipende kazi yake, ili kuokoa maisha ya watu, tuwe wauguzi bora Rais wetu ni Daktari ni lazima na sisi tuende kidaktari kwa manufaa ya wananchi” alisema Waziri.

Aliwataka wauguzi na wakunga kuwajali wagonjwa wote wanaofika kwa ajii ya matibabu, na sio kumjali mtu unaemjuwa na  kumletea dharau mgonjwa usiemjuwa.

Pia aliwasisitiza wakunga na wauguzi kuwajibika vizuri katika majukumu ya kazi zao, na sio kupoteza wakati kwa kuchezea simu muda wakazi na kufanya mazungumzo,  jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kazi.

“Uwajibikaji na nidhamu ndio tunaoutaka, kuingia kazini kwa wakati na kutoka kwa wakati,  na sio kufanya utoro, hilo  halitakiwi”.  alisisitiza Waziri.

Aidha aliwashauri wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa mashirikiano ili waweze kubadilishana uzoefu, kwa lengo la kuhakikisha ufanisi unapatikana kazini, pamoja na kutunza siri za wagonjwa na sio kutoa siri zao.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa hospitali binafsi pamoja na walimu mbalimbali wa vyuo vikuu Nchini.

Loading