ZANZIBAR YAADHIMISHA SIKU YA MALARIA DUNIANI

Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Sulueiman akihutubia wananchi waliojitokeza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani, (kulia) Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Abdalla na kushoto Mkuu wa Wilaya Kaskazini ‘B’ Rajab Ali Rajab.

Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Sulueiman amesema Wizara yake itaendelea kutumia mikakati ya kupambana na malaria ambayo imeonyesha mafanikio makubwa ya kupunguza maradhi hayo ili kuhakikisha maradhi hayo yanaondoka kabisa.

Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, kutumia tiba ya dawa mchanganyiko, kufanya ufuatiliaji wagonjwa majumbani na kuendeleza zoezi la upigaji dawa majumbani katika sehemu ambazo bado wagonjwa wa maradhi hayo wanapatikana.

Naibu Waziri ameeleza hayo katika maadhimisho ya siku ya malaria duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa mpira wa Misuka, Mahonda Wilaya ya Kaskazini B.

Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kupambana na malaria hadi kufikia chini ya asilimia moja lakini bado kuna baadhi ya sehemu hasa katika Wilaya Kaskazini B, Wilaya ya Kati na Wilaya ya Magharibi bado maradhi hayo yapo.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ikishirikiana na wadau mbali mbali zikiwemo taasisi za kitaifa na kimataifa za ndani na nje ya nchi.

Harusi Saidi Suleiman aliwataka wananchi waliopata vyandarua waendelee kuvitumia kikamilifu pamoja na kuvitunza kwani kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji wagonjwa majumbani unaonyesha kuwa matumizi ya vyandarua kwa jamii bado yapo chini.

Aliweka Wazi kuwa Wizara ya Afya itaendelea kutoa vyandarua bila malipo kupitia vituo vya afya kwa mama wajawazito , watoto wenye umri wa miezi tisa na wanajamii kwa jumla.

Aidha aliwakumbusha wananchi kuwa huduma za uchunguzi wa malaria zinapatikana katika vituo vyote vya afya, vikiwemo vituo vya bandarini na uwanja wa ndege ambavyo vimewekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na kutoka Zanzibar.

Katibu Tawala Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Makame Machano Haji akitoa tarifa ya Malaria ya Mkoa wa Kaskazini katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika Mahonda Wilaya ya Kaskazini B.

Akizungumzia hali ya Malaria katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Katibu Tawala Wilaya Kaskazini ‘B’ Makame Machano alisema jumla ya watu 52,356 waliochunguzwa mwaka jana, watu 655 sawa na asilimia 1.3 walibainika kuwa na vimelea vya Malaria na wengi wanatoka Wilaya ya Kaskazini B.

Alisema tatizo la Malaria katika Mkoa huo linachangiwa na kuwepo kwa mazalia ya mbu, muamko mdogo wa wananchi katika kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na wasafiri wanaoingia kutoka nje ya visiwa vya Zanzibar.

Alisema mwaka huu wa 2019 Mkoa wa Kaskazini umepania kuodosha chongamoto zote zinazosababisha kuwepo Malaria mkoani humo na kuongeza taaluma ili jamii iwe na muamko wa mbinu za kujikinga na ugonjwa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Rajab Ali Rajab alisema uongozi wa Wilaya yake ulisimamia kikamilifu zoezi la upigaji dawa majumbani lililofanyika mwezi Machi mwaka huu na wananchi waliokataa zoezi hilo walitumia nguvu kufanikisha kazi hiyo.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani kwa upande wa Zanzibar mwaka huu ”Zanzibar bila Malaria inawezekana”. ‘Mimi na wewe tumalize Malaria Zanziba’.

Loading