MADAKTARI WAKICHINA WAFANYA UPASUAJI KWA NJIA YA MATUNDU

Kiongozi wa timu ya 28 ya Madaktari kutoka China (kushoto) Dkt. Zhang Zhen akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maendeleo ya matibabu Duniani ambayo hivi sasa yanafanyika pia katika  Hospitali ya Mnazimmoja kupitia madaktari wa China kwa mashirikiano na madaktari wazalendo.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Madaktari bingwa kutoka China imewataka wananchi kwenda hospitali ya Mnazi Mmoja kupata huduma muhimu za matibabu ya maradhi ya Mkojo na matatizo ya mishipa ya hisia bila ya malipo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mafunzo na Utafiti Wizara ya Afya Mwinyi Mselem amesema huduma za maradhi hayo zinatolewa katika Hospitali ya Mnazimmoja na hakuna haja ya kufuatilia matibabu nje ya nchi.

Amesema timu ya madaktari bingwa kutoka China wamefanikiwa kutoa huduma za matibabu ya maradhi ya Mkojo, uvimbe mkubwa na matatizo ya mishipa ya hisia (kiharusi) na wagonjwa hao wanaendelea vizuri.

“Kulikuwa na mgonjwa ana saratani na tatizo la haja kubwa madaktari wa kichina walimfanyia upasuaji na kuweza kuondoa tatizo pia kwa kutumia njia ya adpancha wameweza kumtibu mgonjwa aliyekuwa hana hisia ambae hawezi kuzungumza na wafanikiwa na sasa anaendelea vizuri”, alieleza Mkurugenzi huyo

Mkurugenzi Mwinyi amewataka wananchi kuiamini hospitali ya rufaa ya Mnazi mmoja kwa vile huduma zake zimeboreshwa sana na wagonjwa ambao matatizo yao yameshindikana katika vituo vidogo vya afya kuitumia hospitali hiyo.

Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti Wizara ya Afya Zanzibar Mwinyi Msellem (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya madaktari wa China na waandishi wa habari.

Nae Kiongozi wa timu ya Madaktari hao Dk. Zhang Zhen amesema wamefanikiwa kufanya matibabu ya maradhi mbali mbali yaliyokuwa yakionekana hayawezi kutibika Zanzibar.

Amesema timu hiyo imeanzisha Upasuaji kwa kutumia njia ya matundu kuondosha tatizo la Tezi Dume bila ya kupasua sehemu kubwa ambayo ni nzuri na rahisi katika kutoa huduma za mardhi ya aina hiyo.

Timu ya 28 ya madaktari kutoka China yenye madaktari 18 wataendelea kuwepo Zanzibar hadi mwezi Julai mwaka huu na wanatoa huduma katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja na Abdalla Mzee Mkoani na wanasaidia vituo vyengine vya Afya Unguja na Pemba.

Loading