WAKUNGA NA WAUGUZI WATAKIWA KUONGEZA HUDUMA KWA MAMA WAJAWAZITO

Mkuu wa mkoa mjini magharibi ayoub mohd mahmoud amewataka wakunga na wauguzi kuendelea kutoa huduma bora kwa mama wajawazito ili kuhakikisha wanajifungua salama na kupunguza vifo vinavyotokana  na uzazi.

Mh. Ayoub alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wakunga na wauguzi katika maadhimisho ya siku ya wakunga duniani ambayo kwa zanzibar yalifanyika uwanja wa mapinduzi square michenzani.

Aliwataka wafanyakazi hao mbali na kusimamia usalama wa mama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua, pia wanajukumu la kulinda maadili ya kazi zao ya kutotoa siri za wagonjwa wanao wahudumia.

Mkuu wa mkoa alisema serikali inaendelea na juhudi zake za kuweka mazingira bora katika wodi za kujifungulia na kutoa elimu kwa wafanyakazi wa kada tofauti kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. 

Alisema serikali imeimarisha huduma katika vituo vya afya vijijini ili viweze kutoa huduma za mama mtoto hivyo amewashauri mama wajawazito kuvitumia vituo vya karibu ili kupunguza msongomano katika hospitali kuu ya mnazimmoja.

Aidha mkuu wa mkoa alikemea vitendo vya udhalilishaji na ubakaji wanavyofanyiwa wanawake na watoto na kuitaka jamii kushirikiana na serikali katika kupiga vita vitendo hivyo.

Alisema serikali imelazimika kubadilisha sheria katika kuhakikisha watu wanaofanya vitendo hivyo hawapewi dhamana lakini bado vitendo hivyo vinaendelea kufanyika.                     

Akitoa maelezo kuhusu siku ya wakunga duniani, mwenyekiti wa baraza la wauguzi na wakunga zanzibar bi. Amina abdulkadir alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuwaunganisha wafanyakazi wa kada hiyo katika kujipima ili kuona mafanikio na changamoto zinazowakabili.

Alisema hivi sasa mataifa yaliyomo katika ukanda wa afrika mashariki na kati zimekubaliana kuwa mtaala mmoja wa masomo ya wauguzi na wakunga katika kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa sawa katika nchi hizo.                Katika risala yao iliyosmwa na asha kombo khamis wamesema lengo lao ni kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wanawake na watoto na kuwapatia haki zao za msingi.            

Loading