MKUTANO WA 11 WA KUTATHMINI SEKTA YA AFYA WAFANYIKA ZANZIBAR

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa 11 wa kutathmini Sekta ya Afya Zanzibar katika Ukumbi wa Verde Hotel mjini Unguja

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohammed Mahmoud amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuimarisha sekta ya afya na kufikia malengo iliyojiwekea ikiwemo kudhibiti kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria na UKIMWI.

Amesema juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali na Washirika wa maendeleo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuyafanya magonjwa hayo kubaki chini ya asilimia moja.

Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa 11 wa kutathmini sekta ya Afya kwa mwaka 2017/2018 uliofanyika Ukumbi wa Hotel ya VERDE, mjini Zanzibar.

Amesema ana matumaini makubwa kuwa baada ya kipindi kifupi Ugonjwa wa Malaria utakuwa jambo la kihistoria ambalo Vizazi vinavyokuja vitasimuliwa.

Amefahamisha kuwa mwaka 2003 kiwango cha Malaria kilikuwa asilimia 40% Zanzibar lakini mwaka 2017 kiwango hicho kimeshuka hadi chini ya asilimia moja.

Muakilishi wa W.H.O Zanzibar Dkt.Ghirmany Andermichael akizungumza katika Mkutano wa 11 wa kutathmini Sekta ya Afya Zanzibar katika Ukumbi wa Verde Hotel mjini Unguja

‘‘Ndugu washiriki naomba niwe mtu wa mwanzo kukwambieni kuwa kwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali yetu chini ya Dk. Shein muda si mrefu ugonjwa wa Malaria utakuwa historia ambayo Vizazi vyetu vitajifunza, kubwa tuendelee kuzidi kushirikiana kwa pamoja’’ alinasihi Mkuu wa Mkoa.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba Washirika wa Maendeleo kuendelea kutoa misaada yao kwa Zanzibar ili kutimiza malengo yaliyojiwekea.

Mkuu wa Mkoa amewasisitiza washiriki wa Mkutano huo kubuni njia zitakazosaidia kuwahamasisha Makadtari na wahudumu wa Afya kufanya kazi vijijini badala ya kukimbilia mijini.

Aidha amewaomba wafanyakazi wa Afya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya bila kujalisha hali ya kipato chake wala eneo analotoka.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla akitoahotuba yake katika Mkutano wa 11 wa kutathmini Sekta ya Afya Zanzibar katika Ukumbi wa Verde Hotel mjini Unguja

Kwa upande wake Katibu mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdulla alisema kwa sasa huduma za afya zimeimarishwa Zanzibar ambapo kila eneo la kilo mita tano kuna kituo cha afya ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma hizo.

Aliipongeza Serikali kwa kutekeleza Sera ya Ugatuzi ambapo Wizara hiyo inafanyakazi kwa karibu kuwafikia wananchi wote wa Zanzibar kupitia Ugatuzi.

Hata hivyo Katibu huyo alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana bado Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya Maradhi yasiyoambukiza hali inayowafanya Wadau wake kutumia muda mwingi kukabiliana na maradhi hayo.

Aliyataja maradhi hayo kuwa ni pamoja na Shinikizo la Damu, Kisukari na Saratani ambayo Wizara ya Afya kupitia kitengo cha kupambana na maradhi yasiyoambukiza inafanya jitihada kubwa ya kuelimisha jamii ili kujua namna ya kujikinga.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud katikati akiwa na Naibu Waziri Wizara ya Afya Harusi Saidi Suleiman(kushoto yake)na Viongozi mbalimbali katika Picha ya pamoja katika hafla ya Mkutano wa 11 wa kutathmini Sekta ya Afya Zanzibar katika Ukumbi wa Verde Hotel mjini Unguja.
Loading