ZFDA YATEKETEZA TANI 106 ZA BIDHAA MBALIMBALI ZISIZOFAA KWA MATUMIZI YA BINADAMU

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Dkt. Kahamis Ali Omar akizungumza na Wanahabari hawapo pichani kuhusu zoezi la kuteketeza bidhaa mbali mbali zilizoharibika huko Kibele Mkoa wa kusini Unguja.

Jumla ya Tani 106 za Bidhaa mbali mbali ikiwemo Mchele zimeteketezwa na Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) baada ya kubainika hazifai kwa matumizi ya Binadamu.

Zoezi la kuteketeza bidhaa hizo limefanyika Jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Uguja na kusimamiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Dkt. Kahamis Ali Omar.

Akizungumza na Wanahabari wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo Dkt. Khamis alisema lengo la uteketezaji wa bidhaa hizo ni kuzizuia zisiingie katika mzunguko wa Soko na kwenda kuathiri Wananchi ambao wangezitumia.

Amezitaja bidhaa hizo kutoka Makampuni tofauti kuwa ni pamoja na Mchele, Juice, Tomato, Maziwa, Dawa za Mbu na Pempus za Watoto ambazo zote ziliingizwa kutoka nje ya nchi.

“Kiujumla bidhaa nyingi zimeharibika kutokana na mzungungo wa usafiri ambazo zingine ziliingia maji chunvi ikiwemo Mchele, Juice na Maziwa na baadhi ndio zimepitwa na muda” alisema Dkt. Khamis

Dkt. Khamis amesema wapo Wafanyabiashara ambao wameanza kuelewa umuhimu wa mashirikiano na ZFDA na hivyo kuitaarifu ofisi yao pale bidhaa zao zinapopata hitilafu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Ametoa wito kwa Wafanyabiashara wengine kutoa ushirikiano na ZFDA ili kuendelea kuingiza bidhaa ambazo zinaviwango kwa faida ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Ushauri wangu kwa wafanyabiashara pale bidhaa zao zinapoharibika basi waje moja kwa moja ofisini kwetu ili tuchukue hatua za kuziangamiza kwa ushirikiano” alinasihi Dkt. Khamis

Wafanyakazi wa ZFDA wakipasua vipolo vya Mchele kwa ajili ya kuuteketeza, katika zoezi lililofanyika Jaa la Kibele Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Hata hivyo alisisitiza kuwa watashirikiana vyema na Wafanyabishara waaminifu lakini wale ambao watakua wanakiuka taratibu ZFDA itawachukulia hatua za kisheria.

Amefafanua kuwa katika kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi mkubwa hushirikina na wadau mbali mbali ikiwemo Maafisa kutoka Idara ya mazingira.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa ZFDA alitoa wito kwa Wananchi kuwafichua wafanyabishara wanaouza bidhaa zilizopitwa na wakati na wale wote wenye Ghala za kinyemela ili kuwachukulia hatua za kisheria.

Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) umekuwa ukifanya juhudi mbalimbali ikiwemo kuwasimamia Wafanyabishara ili kuingiza Bidhaa nchini zenye ubora ambazo zitakuwa hazina madhara kwa watumiaji.

Loading