JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAFANYA SEMINA YA KUTENGENEZA MWONGOZO WA PAMOJA WA KUTATHIMINI MATUMIZI YA DAWA ZANZIBAR

Wananchi wametakiwa kuzitumia Dawa vizuri kwa kufuata kikamilifu miongozo wanayopatiwa na Wataalam wa Afya ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kupitia Dawa hizo.

Aidha wameombwa pale yatakapotokea madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kuripoti haraka kwa Wataalam wa Afya ili hatua za matibabu ziweze kuchukuliwa.

Mkurugenzi wa Bohari kuu ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad ameyasema hayo alipokuwa akifungua Semina ya siku mbili ya kutengeneza Mwongozo wa pamoja wa kutathimini matumizi ya Dawa kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki katika Hoteli ya Marumaru mjini Zanzibar.

Amesema matumizi ya Dawa yanahitaji umakini mkubwa ili kuepuka madhara zaidi kwa wagonjwa wanaotumia Dawa.

Amesema kutokana na hali hiyo Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika imeona ipo haja ya kuwa na mwongozo mmoja ambao utahakikisha Wananchi wanakuwa salama dhidi ya matumizi ya Dawa.

“Dawa si chakula, Dawa ni Sumu, ukiitumia vyema kwa kufuata miongozo yake itakutibu lakini kama utaitumia vibaya kinyume na inavyotakiwa basi itakuletea madhara” alitahadharisha Zahran

Amefahamisha kuwa watu wanaweza kupata matatizo mbali mbali pale wanapotumia Dawa bila kufuata mwongozo sahihi kama vile kupata muwasho na baadhi ya wakati hata kusababisha madhara ndani ya mwili hivyo umakini unahitajika.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Uwiano wa Dawa wa nchi za Afrika Mashariki Hidaya Juma, amesema kupitia Mradi huo wameweza kutengeneza miongozo tofauti ikiwemo ya usajili wa Dawa, kupima ubora wa dawa zenyewe na kuvifanyia ukaguzi Viwanda vya Dawa vya Afrika Mashariki.

Bi Hidaya ameongeza kuwa malengo ya Mkutano huo ni kuhakikisha Dawa zote zinazoingia nchi wanachama wa Afrika ya Mashariki ziwe katika kiwango kimoja cha ubora.

Amesema mara baada ya kukalmilika Mradi huo wataweza kuweka hali ya Dawa kuwa na usalama Afrika Mashariki

Hivyo amesisitiza Wananchi pale wanapopata tatizo linalotokana na matumizi ya Dawa walizozitumia kuliripoti tatizo hilo kwa wahusika.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa Semina hiyo Mohamed Omar Simba amesema Mwongozo huo baada ya kukamilika utawasaidia kuwapa uelewa mpana wa kujua namna ya kuzitumia vyema Dawa hizo kwa matumizi.

Amesema Wataalam wamegundua kwamba baadhi ya Wagonjwa wanaoletwa Hospitalini kwa matibabu magonjwa yao hutokana na matumizi mabaya ya dawa.

Afisa mwandamizi wa Afya kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki Jane Mashingia amesema wamekuja kuchukua maoni ya Wadawau wanaofanya kazi za kutoa Dawa kutoka taasisi tofauti ikiwemo Wasambazaji wa Dawa, Watengenezaji wa Dawa na Mamlaka ya kudhibiti ubora wa Dawa Zanzibar ZFDA.

Ameongeza kuwa zoezi la kukusanya maoni ili kutengeneza mwongozo huo limeanza nchi tofauti kama vile Kenya, Uganda, Tanzania Bara ambapo kwa sasa wapo Zanzibar kabla ya kuhitimishwa katika nchi zilizobaki za Burudi, Rwanda na Sudan Kusini.

Loading