WIZARA YA AFYA ZANZIBAR YAAHIDI KUENDELEZA TAFITI ZA TIBA ASILIA

Mkurugenzi Mkuu wa Tasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar Dkt. Mayassa Salum ally akimpa maelezo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tianjin cha China Prof. Bian Yuhong katika Mkutano wa siku moja wa utafiti wa Tiba asilia.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mnazimmoja Dk. Ali Salum Ali amesema Wizara ya Afya itaendelea kufanya utafiti aina mbali mbali za mimea iliyopo Zanzibar ili kuzalisha dawa mpya za Tiba Asilia kwa ajilia ya kutibu maradhi mbali mbali.

Akizungumza katika mkutano wa Tafiti wa Tiba asilia ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) na kuwashirikisha wadau wa tiba hiyo na ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Tianjin cha China, Dk. Ali alisema dawa nyingi zinazotumika Hospitali zinatokana na mimea baada ya kufanyika tafiti mbali mbali za kisayansi.

Alisema kutokana na kutambua umuhimu wa mimea kwa ajili ya Tiba asilia, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na watibabu wa tiba hiyo ambao wanatumia mizizi, majani na magome ya mimea.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mnazimmoja aliweka wazi kuwa Zanzibar imepiga hatua katika matibabu ya Tiba asilia na sehemu nyingi watibabu wa tiba hiyo wanapatikana hivyo kitu muhimu ni kuongeza wigo wa kufanya Tafiti.

Alisema kutokana na umuhimu wa Tafiti kwa maendeleo ya Taifa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha vitengo vya utafiti kwa kila Wizara na kuanzisha Taasisi maalumu ya masuala ya afya ili kuona kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) Dk. Mayasa Salum Ali alisema Watibabu wa Tiba asilia wanatoa mchango mkubwa kusaidia jamii katika matatizo mbali mbali ya kiafya yanayowakabilili na kuyapatia ufumbuzi.

Alisema iwapo wananchi wote wanaopata matatizo ya afya wangeenda Hospitali na vituo vya afya kutafuta matibabu visingeweza kukidhi mahitaji lakini mchango wa Watibabu wa Tiba asilia ni mkubwa na unathaminiwa.

Aliahdi kuwa ZAHRI itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa Tiba asila na wananchi wa mijini na vijijini kuhakikisha lengo la kuundwa kwa Taasisi hiyo linafanikiwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tianjin cha China Prof. Bian Yuhong akitoa mada kuhusu matibabu ya Tiba asilia nchini China

Mhadhiri wa Kitivo cha Afya kutoka Chuo Kikuu cha Tianjin cha China Prof. Yuhong Bian alisema WHO  imeweka mipango endelevu ya Kidunia na Kikanda katika kukuza na kuendeleza Tiba asilia kutokana na kutambua mchango wake kwa wananchi.

Alisema China ni moja ya nchi zinazothamini na kuendeleza matibabu ya Tiba asilia kwa miaka mingi na ziko Hospitali na Taasisi kubwa zinazotoa matibabu hayo na wananchi wanaziamini na wanaendelea kuzitumia kwa matatizo mbali mbali ya afya zao.

Loading