WANANCHI WATAKIWA KUFANYA JITIHADA BINAFSI KUJIKINGA NA SARATANI

Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maradhi ya Saratani Zanzibar Dkt. Msafiri Marijani akitoa taarifa ya ukubwa wa maradhi ya Saratani kwa waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Saratani Duniani yaliyofanyika Ofisi ya Jumuiya ya Maradhi yasiyoambukiza Mpendae, (kulia ) Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman.

Wananchi wametakiwa kubadili mfumo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kutumia kiasi kidogo cha mafuta na kuepuka matumizi ya Pombe na Tumbaku ili kujikinga na maradhi ya Saratani.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman katika hafla ya maadhimisho ya siku ya Saratani Duniani huko ukumbi wa Kituo cha Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Z-NCDA Mpendae mjini Zanzibar.

Amesema kumekuwa na ongezeko la maradhi hayo Zanzibar na Dunia kwa ujumla na hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kuzuia kasi ya maradhi hayo isiendelee.

Naibu Waziri amefahamisha kuwa kwa mujibu wa Takwimu zilizopo Hospitali ya Mnazi mmoja mwaka 2015 Wagonjwa wapya wa Saratani waligundulika 271. Mwaka 2016 waligunduliwa 392 ambapo mwaka 2017 waligunduliwa wagonjwa 560.

Hivyo amesema jitihada za kuelimisha jamii juu ya kujikinga na maradhi ya Saratani zinapaswa zifanywe kila muda kunusuru Maisha ya Wananchi.

Zamani kila mtu kwa nafasi yake aliweza kuelezea madhara ya ugonjwa wa UKIMWI na watu wakafahamu kwa hiyo imefika muda wa kuyajadili maradhi yasiyoambukiza ikiwemo Saratani kila sehemu katika baraza na vikao vyetu ili watu wajue namna ya kujikinga” alisema Bi. Harusi.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya saratani Duniani yaliyofanyika Ofisi ya Jumuiya ya maradhi yasiyoambukiza Mpendae Mjini Zanzibar

Naibu Waziri huyo amefahamisha kuwa Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua juhudi mbalimbali za kukabiliana na maradhi ya Saratani ikiwemo kuhakisha upatikanaji wa Dawa na kuwaongezea ujuzi Wataalam wa Saratani.

Aidha alishauri kuwepo kwa mikakati mbalimbali ya kupunguza maradhi hayo ambayo huipa mzigo mkubwa Serikali kwa matibabu ya Wananchi wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Maradhi ya Saratani Zanzibar Dkt. Msafiri Marijani amesema kinga ya maradhi hayo haipo serikalini badala yake ni juhudi binafsi za mtu mmoja mmoja kuepuka vichocheo vya maradhi hayo.

Amefahamisha kuwa pale Wananchi watakapokula vyakula bora na kufanya mazoezi ipasavyo watakuwa wamejiweka katika mazingira salama ya kujikinga na Saratani.

Amezitaja aina za Saratani zinazoongoza kwa kusababisha vifo Zanzibar kuwa ni Saratani ya Tenzi Dume ambayo huwakumba Wanaume na Saratani ya Shingo ya Kizazi na Matiti ambazo huwakumba wanawake.

Hivyo amewataka wananchi kufanya uchunguzi wa mara kwa mara Hospitalini ili kuyagundua mapema maradhi hayo na kupata tiba sahihi na kwa wakati sahihi.

Kila ifikapo February 4 Zanzibar huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya Saratani ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Naweza na pamoja tunaweza kupunguza Vichocheo na gharama za maradhi ya Saratani’’

Loading