Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdallah na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa ya MOI Dkt. Respicious Boniface wakibadilishana hati baada ya kutia saini makubaliano ya wagonjwa wa Mifupa wa Zanzibar kutibiwa Taasisi hiyo. Hafla ya utiaji saini ilifanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya afya Asha Ali Abdalla amesema mashirikiano ya huduma za afya kati ya Wizara ya Afya na Taasisi ya Mifupa ya MOI kutasaidia kupunguza gharama kubwa ya matibabu ya wagonjwa wa mifupa kupelekwa nje ya Tanzania.
Aliyasema hayo katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja wakati wa utiaji saini makubaliano ya kuwapeleka wagonjwa wa mifupa wa Zanzibar kutibiwa katika Taasisi ya MOI.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla alitia saini kwa niaba ya Wizara ya Afya Zanzibar na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa ya MOI Dkt. Respicious Boniface aliiwakilisha Taasisi hiyo.
Alisema lengo la mashirikiano hayo ni kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa wenye matatizo ya mifupa nje ya Tanzania ambazo zimekuwa zikiongeza kila mwaka.
Aidha alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa mifupa kutokana na ajali mbalimbali ambazo hutokea bila kutegemewa .
Alifahamisha kuwa maradhi ya mifupa pia yamekuwa tatizo kubwa kwa wananchi wengi wenye umri mkubwa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa ya MOI Dkt. Respicious Boniface amesema makubaliano hayo yataongeza ushirikiano uliopo wa huduma za afya hasa ukizingatia Taasisi hiyo imepiga hatua kubwa kitaalamu katika kutibu maradhi ya mifupa na magonjwa mengine ya aina hiyo.
Aidha alisema mashirikiano hayo yatasaidia kupunguza changamoto za kuchelewa kupatiwa matibabu wanaopata ajali na kutarahisisha kupata matibabu kwa wakati muafaka .
“Tutashirikiana pamoja ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na kwa haraka na kusaidia kutoa tiba kwa watanzania kwa ufanisi,” alisema Mkurugenzi wa MOI.
Mkurugenzi huyo alisema huduma za matibabu ya upasuaji mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu katika Taasisi ya MOI zimeimarishwa ili kutoa huduma bora zaidi kwa jamii .
Alieleza sehemu ya maabara zimewekwa mashine mpya na za kisasa, vyumba vya upasuaji vimeimarishwa na kuna mashine za kisasa ICU na kuongeza vitanda vya upasuaji.