Wizara Ya Afya yatiliana saini mkataba wa kuipatia hospitali ya Mnazimmoja vifaa vya kutibu mifupa

Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto  inakusudia kujaza vifaa tiba kamili katika kitengo cha matibabu ya mifupa kilichoko katika hospitali ya rufaa Mnazimmoja mjini Zanzibar.

Hatua hiyo inalenga kutoa huduma za uhakika kwa wagonjwa wenye mahitaji ambao hufika hospitalini hapo.

Mkurugenzi tiba wa wizara hiyo Dkt. Juma Salum Mbwana, amesema katika hafla ya kutiliana saini na kampuni ya Brett and Bgleystif Ltd ya Dar es Salaam, kuwa huo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili kuondoa malalamiko ya wananchi juu ya upatikanaji huduma bora.

Mkurugenzi huyo aliyekuwa akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, alisema tayari mkataba huo umeanza kutekelezwa kwa baadhi ya vifaa hospitalini vinavyoendelea kuwekwa katika kitengo cha matibabu ya mifupa.

Alifahamisha kuwa, hatua hiyo pia ni faraja baadhi ya wagonjwa ambao wamekuwa wakikosa matibabu kutokana na kutokuwepo vifaa vya kutosha katika hospitali hiyo ambayo ni kimbilio la wananchi wengi.

Aliishukuru Serikali kwa kuwapangia mikakati maalum itakayoweza kukidhi mahitaji ya wagonjwa na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Dkt. Gabriel kutoka Dar es Salaam, alisema lengo la mkataba huo wa miaka  mitatu ni kuwasaidia wagonjwa wanaopata ajali pamoja na watu wazima wenye matatizo ya kuumwa na nyonga.

Aidha, alieleza kuwa msaada huo wa kitaalamu utaisaidia serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazika katika ununuzi wa vifaa kwani huduma zitolewazo ni za kisasa ambazo hazihitaji mgonjwa  kufanyiwa upasuaji.

Kwa upande mwengine, Dkt. Gabriel amewataka madaktari wa hospitali ya Mnazimmoja kushirikiana kwa pamoja ili kufikia lengo lililokusudiwa katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Naye  Dkt. Hamid Masoud, bingwa wa upasuaji mifupa katika hospiali hiyo, alisema kutakuwa na kitengo maalum cha kuhifadhia vifaa hivyo ili vidumu na kutumika kwa muda mrefu sambamba na kuondosha malalamiko kutoka kwa baadhi ya madaktari.

Alizitaja hospitali zilizokwisha kupatiwa vifaa hivyo nchini Tanzania, kuwa ni KCMC, CCBRT, MOI, TMJ, Kairuki, Selian (ALMC), Rabinninsia na Benjamin Mkapa.

Loading