SPIKA WA BARAZA LA WAWAKILISHI AWEKA JIWE LA MSINGI MAABARA YA WAKALA WA CHAKULA DAWA NA VIPODOZI ZANZIBAR

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid amewataka Wakurugenzi wa Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi  na Bodi yake  kuzidisha juhudi katika kudhibiti uingiaji wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binaadamu .

Amesema kufanya hivyo kutasaidia kudhibiti uingiaji wa bidhaa zisizofaa nchini na kuhakikisha bidhaa na huduma zinazotolewa zinakuwa katika viwango vya ubora na usalama vilivyowekwa kitaifa na kimataifa

Kauli hiyo aliitowa wakati wa uwekaji wa jiwe la Msingi la Jengo la Maabara za Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi (ZFDA) huko Mombasa Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za Sherehe ya Miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar .

Amesema mara baada ya Mapinduzi ya Matukufu ya Januari 12 mwaka 1964 Serikali ya Afro Shirazi ilikuwa ikitoa huduma za afya bure kwa wananchi sambamba na kuagiza na kusambaza chakula na dawa hivyo masuala yote ya ubora wa usalama wa bidhaa za chakula kupitia Shirika la Bizanje  na dawa Wizara ya Afya

Aidha alisema jukumu la serikali ni kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa kwani ni msingi mkubwa wa maendeleo katika taifa  kwa lengo la kuweza  kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa kama vile kilimo ufungaji uvuvi biashara ,kufanyakazi ofisini pamoja na viwandani.

Hata hivyo aliwashukuru wahisani ambao walishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kuwaunga mkono na kutekeleza ahadi zao  pamoja na kutoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Dr Ali Mohammed shein Rais Mstaafu wa awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuridhia kuanza kwa ujenzi wa maabara hiyo .

Nae  Kaimu Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Mheshimiwa, Simai Mohammed Said  alitoa nasaha kwa wafanyabiashara kwa kuwataka kuleta bidhaa zilizokuwa nzuri na zenye kufikia kiwango ili  kutimiza jukumu lao la kumlinda malaji .

Alifahamisha kuwa mfanyabiashara atakapotekeleza jukumu hilo litamsaidia kuepuka gharama za kutakiwa kuzirudisha bidhaa zilikotoka au kuziteketeza ambazo kwa kawaida hulazimika kuzichukua endapo wakileta bidhaa zisizofaa kwa matumizi

Pia aliwasihi wafanyakazi na watendaji wa wakala wa chakula dawa na vipondozi na serikali kwa ujumla kuwa waadilifu katika kutekeleza kazi zao na kujuwa kwamba wanawajibu mkubwa katika kutekeleza jukumu la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kulinda afya za wananchi

Mapema Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Halima Maulid Salum alisema wakala wa chakula dawa na vipodozi zanzibar (ZFDA)ni miongoni mwa wakala wa serikali iliopo chini ya wizara ya afya yenye dhima ya kusimamia na kudhibiti ubora na usalama wa bidhaa na chakula dawa vifaa na utibabu kwa kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa na kuingizwa nchini zinakuwa salama na zenye  viwango vinavyokubalika ili kulinda afya za wananchi.

Alisema Ujenzi wa jengo la maabara ya wakala wa chakula dawa vipodozi Zanzibar unatekeleza kwa awamu mbili awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa jengo la horofa tatu  sambamba na uwekaji wa miundombinu ya maabara na awamu ya pili itahusisha uwekaji wa vifaa vya maabara.

Gharama za Utekelezaji wa mradi huu wa awamu zote ni shilingi za Tanzania bilioni 4.8 kati ya fedha hizo serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imetoa shilling za Tanzania bilioni 3.3 za utekelezaji wa awamu ya kwanza na kwa awamu  pili shilingi za Tanzania bilioni 1.5 zinatarajiwa kutoka wahisani kupitia jumuiya ya afrika mashariki na Mradi wa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika machi 2021

Loading