Ujumbe wa Maendeleo na Utetezi Duniani wakutana na Waziri wa Afya Zanzibar

Ujumbe wa Maendeleo na Utetezi Duniani (Global Development and Advocacy) umesema utaendeleza mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya afya ili kuhakikisha athari za maradhi yasioambukiza zinapungua nchini. 

Hayo ameyasema Mkuu wa Maendeleo na Utetezi Duniani Mr.Bent Lautrup – Nielsen kutoka Denmark wakati akizungumza na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee,Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui katika hafla fupi ya mazungumzo ya miradi ya maendeleo huko Ofisini kwake Mnazimmoja .

Amesema maradhi yasioambukiza ni tatizo kubwa linaloathiri duniani kote hivyo iko haja ya kushirikaina ili kuyadhibiti maradhi hayo yasiendelee kuiathiri jamii .

Aidha ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukubali kufanyika Mkutano wa kimataifa hapa Zanzibar katika mwaka 2023 ili kuihamasisha jamii jinsi ya kuyadhibiti na kujikinga kwa kufuata maelekezo ya wataalamu .

Nae Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui ameishukuru ujumbe huo kwa kuwapatia dola za kimarekani laki 782,000 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo vifaa tiba ambavyo vitasaidia kudhibiti maradhi hayo .

Aidha amesema vifaa hivyo ni pamoja na gari moja, mashine ya kuchunguza athari za vidonda kwa mgonjwa wa sukari kabla ya kujitokeza pamoja na mashine ya kusaidia mgonjwa wa kisukari ambaye kapoteza nuru ya macho ili kuweza kuona  .

Alisema Shirika la Maendeleo na Utetezi Duniani inafanya kazi zao hapa Zanzibar kwa muda wa mwaka wa 20 kwa kuisaidia Zanzibar kwa kutoa mashine madawa na wafanyakazi wa afya kupata nafasi ya kusoma nje ili kuzidisha utaalamu.

Wakati huu huo Mwenyekiti wa Umoja wa Mahoteli Paolo Rosso alitoa shukrani kwa Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii,Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui kwa kuwapatiwa wafanyakazi wa mahoteli chanjo ya uviko 19 .

Loading