TUSHIRIKIANE KUPAMBANA NA UGONJWA WA KISUKARI – MHE. OTHMAN

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema maradhi yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya kisukari bado yanabaki kuwa tishio kwa afya ya jamii na dhidi ya maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani, iliyofanyika katika Viwanja vya Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi (Mapinduzi Square), Kisonge Jijini hapa.

Amesema kasi ya magonjwa yasiyoambukiza hapa visiwani ni changamoto kubwa, na inayopelekea athari za ziada kwa wanaougua maradhi mengine yakiwemo ya UVIKO-19, na pia kuchochea ongezeko la watu wenye ulemavu hapa nchini.

Akizindua rasmi Zoezi la Siku Kumi na Mbili la Kuhamasisha Chanjo ya UVIKO-19 mijini na vijijini, linalosimamiwa na Wizara ya Afya kwa mashirikiano na wadau mbali mbali wa maendeleo, Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa watu kujenga utamaduni wa lishe bora, kufanya mazoezi, kuelimisha, kuchanja, na kuzingatia kula kwa ustaarabu.

Mh.Nassor Ahmed Mazrui – Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, ameeleza namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyothamini mchango mkubwa na mashirikiano kutoka kwa wananchi na washirika mbali mbali wa maendeleo, katika kuimarisha sekta ya afya hapa visiwani.

Naye Mwakilishi wa AMREF, ambaye ni miongoni mwa wadhamini wa maadhimisho hayo, Dokta Edwin Kilimba ameeleza azma ya Shirika lake ni kuungamkono juhudi zote za kuhamasisha utekelezaji wa malengo na mipango ya Wizara ya Afya Zanzibar kwa kadiri itakavyohitajika.

“Kwa niaba ya AMREF na wahisani wetu tunasema sisi tutakuwa tayari kusaidia na kufadhili miradi na mahitaji yoyote ambayo Wizara ya Afya watatuletea na ambavyo Serikali ya Zanzibar watahitaji kusaidiwa”, amesema Dokta Kilimba.

Maadhimisho hayo yaliyojumuisha viongozi na wadau mbali mbali wa sekta ya afya, yalihusisha maandamano ya wanamazoezi, Bendi ya Kikosi cha Mafunzo, upimaji wa afya wa magonjwa yasiyoambukiza na chanjo ya UVIKO-19,yakiwa na kaulimbiu ‘IMARISHA UPATIKANAJI WA HUDUMA BORA KWA WAGONJWA WA KISUKARI’ .

Loading