WAZIRI WA AFYA AKUTANA NA MKURUGENZI MKAAZI USAID NA UJUMBE WAKE

Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Wazee , jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Mkurugenzi Mkaazi USAID Nchini Tanzania Kate Somrongsiri na Ujumbe wake  mara walipofika Ofisini kwake na kufanya mazungumzo kuhusu miradi mbalimbali ya afya .

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, ameahidi kuilinda na kuiendeleza miradi mbalimbali ya huduma za afya ilioanzishwa na Shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID) ili kuimarisha huduma za afya nchini.

Alitoa ahadi hiyo, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la misaada la watu wa Marekani nchini Tanzania (USAID) Kate Samrongsiri, alipofika  ofisi kwake Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Alisema kuwa, shirika hilo limeweza kuisadia Zanzibar katika miradi mbalimbali ya afya ikiwemo mradi wa kupambana na corona na  kutokomeza malaria, miradi ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa visiwani hapa.

Waziri Mazrui alimueleza Mkurugenzi huyo kuwa, miradi mbalimbali iliofanywa na shirika hilo itaendelea kuthaminiwa, kuenziwa na kulindwa pamoja na kuendelezwa ili wananchi waendelee kunufaika.

“Miradi hii itaendelea kushughulikiwa na serikali na ninaahidi kuwa itaendelezwa na haitoporomoka na tutaendelea kufanya kazi bega kwa bega na shirika hili” alisema Waziri.

Aidha alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika hilo, kwa kuisaidia serikali katika mikakati ya kuboresha sekta ya afya, na kuahidi kuendelea kushirkiana kwa karibu ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana nchini.

Nae Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) Tanzania, Kate Samrongsiri amesema ameridhishwa na jitihada zinazofanywa na serikali za kuendeleza miradi mbalimbali ilioanzishwa na shirika hilo hasa mradi wa kutokomeza malaria visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi huyo alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali ya Zanzibar katika jitihada za kupambana na ugonjwa wa corona pamoja kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa nchini.

Aidha alisema Shirika litaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali ili kuondoa changamoto katika sekta ya Afya, na kuhakikisha jitihada  zinazofanywa na Serikali za kupambana na maradhi mbalimbali zinafanikiwa.

Nae Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya, Dkt Ali Nyanga, alisema Shirika hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha utoaji wa chanjo ya corona kwa Raia na wageni wanaoingia na waliopo nchini.

Alisema kupitia msaada wa Shirika la Watu wa Marekani(USAID)  wameweza kutoa elimu ya ugonjwa wa corona, pamoja na uhamasishaji wa chanjo ya ugonjwa huo Mijini na Vijjiini, jambo ambalo limesaidia katika kuiweka Zanzibar salama.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wanachi wa Zanzibar na wageni wanaongia nchini kuendelea na jitihada mbalimbali za kujikinga na magonjwa mbalimbali ya mripuko.

Loading