Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dk,Jamala Taib akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Shahada ya kwanza ya Uuguzi na Ukunga chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA katika Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba hafla iliofanyika katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Taifa Suza kampasi ya Vuga Zanzibar
Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dkt Jamala Adam Taib ameutaka Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA ) kuhakikisha wanapokea wanafunzi wenye sifa zinastahiki kujiunga na Chuo hicho jambo ambalo litasaidia kutoa wahitimu wenye kiwango bora .
Akiyasema hayo huko katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Vuga, wakati wa Uzinduzi wa Shahada ya Kwanza kwa Uuguzi na Ukunga.
Alisema wanafunzi ambao wanasifa kulingana na kiwango chao cha ufaulu ndio wanaostahiki kujiunga na chuo katika kada ya uuguzi na ukunga kwa lengo la kupata ufaulu wenye hadi na kiwango bora .
Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein aliunganisha vyuo mbali mbali ikiwemo chuo cha afya kwenda Chuo cha Taifa kwa lengo lakuleta msukumo wa kuzipandisha hadhi kada mbali mbali ili kuweza kufikia malengo ya kitaaluma .
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Amina Abdukadir Ali amewataka waunguzi na wakunga kuwa imara katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwasaidia wananchi.
“Mfanyekazi kwa kuwahudumia wananchi kuimarisha hadhi na ubora kiafya muhakikishe hakuna mtu anaeachwa nyuma kupatiwa huduma za afya ikiwemo mama na watoto sio wakati wa masihara ni wakati wa kuleta mabadiliko. “alisema Mwenyekiti huyo.
Aidha aliwataka Wauguzi na Wakunga kuwa na tabia nzuri ya kunyenyekea wagonjwa kwa kufuata maadili na sheria za kazi ili wasiingie katik matatizo .
Kwa Upande wa Naibu Makamo Mkuu wa Chuo cha Taifa (SUZA) Dk Haroun Maalim aliwapongeza wanafunzi kwa kujiunga katika fani ya uuguzi na ukunga fani ambayo hapo awali ilikuwa ikizaraulika .
Alisema hadi sasa wamepokea jumla ya wanafunzi 29 kwa awamu ya mwanzo ya Shahada ya Kwanza kwa Uuguzi na Ukunga ambao wanatarajia kuanza masomo yao .
Nae Mrajisi wa Baraza la Wauguzi Vuai Kombo Haji amesema fani ya uunguzi na ukunga ni ya muda mrefu kwa upande wa Zanzibar imeanza katika mwaka 1938 hadi sasa, ulianzia katika ngazi ya cheti , stashahada hadi sasa inaanzishwa Shahada ya Kwanza ya uuguzi na ukunga .
Fani ya uuguzi na ukunga ifikapo 2020 itaadhimisha kutimiza miaka 200 katika kada ya uuguzi na ukunga duniani