WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR HAMAD RASHID AZUNGUMZA NA WAANDISHI

Waziri wa Afya Hamad Rashid akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Maradhi ya Korona yalioingia katika baadhi ya Nchi Duniani ambapo hadi sasa Zanzibar na Tanzania kwa Jumla hakuna maradhi hayo na kuelezea Tahadhari za kujikinga zilizochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na madawa na Vifaa vya kujikingia hafla iliofanyika ukumbi wa Wizara hio Mnazi mmoja Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imezuia uingiaji wa ndege za kitalii kutoka nchini Italy kuja Zanzibar ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa maradhi ya Corona.

Akizungumza na waandishi wa Habari Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed huko katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja kuhusu mwenendo wa maradhi ya Corona yaliyosambaa Ulimwenguni amesema wamezuia uingiaji wa ndege hizo ili kuchukua tahadhari na ugonjwa huo usisambae nchini.

Alifahamisha kuwa hadi sasa zaidi ya nchi 85 za Umoja wa Mataifa zimeshaathirika na Virusi vya ugonjwa huo hivyo jamii inapasa kuchukua tahadhari kujikinga na kuwa makini na usambazaji.

Waziri Hamadi aliwataka wananchi kuchukuwa tahadhari kuhakikisha wageni wote wanaowasili nchini kufuata taratibu na masharti yaliyowekwa ili kuweza kudhibiti na kuepuka kusambaa nchini.

Waziri huyo wa Afya alisistiza kusitishwa shughuli zote ambazo zinahusisha mkusanyiko wa wageni kutoka nje ya nchi pamoja na wananchi kusafiri katika nchi ziliathirika na ugonjwa huo kwa lengo kulinda usalama wa maambukizi.

Hata hivyo alikemea tabia ya baadhi ya wananchi kuvumisha habari zisizo sahihi kutokana na maradhi hayo, hivyo ameitaka jamii kusikliza taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari ili kujua maendeleo na uhakika wa taarifa hizo kwa lengo la kuwaondolea hofu.

“Zanzibar ugonjwa huu bado haujaingia ila wananchi wawe na tahadhari maalum ili kujikinga”, alieleza Waziri Hamad.

Alifahamisha kuwa serikali tayari inachukua tahadhari kwa kuweka mfumo wa kinga wa udhibiti katika Viwanja vya Ndege na maeneo ya Bandari wananchi wanaoingia nchini wanafanyiwa vipimo pamoja na kuundwa timu  pamoja kutenga eneo maalum katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja na Kidimni kwa ajili ya wagonjwa na watakaogundulika na ugonjwa huo .

Aidha Waziri Hamad aliipongeza Ofisi ya Mufti kwa kuzuia  Ijitimai ya Kitaifa iliyotarajia kufanyika nchini pamoja na sherehe za wageni (Fullmoon Part) kwa wageni kwa lengo la kuchukua tahadhari ya maradhi ya Corona.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk Fadhil Mohamed Abdalla akijibu baadhi ya maswali yalioulizwa na Waandishi wa Habari kuhusiana na Maradhi ya Korona yalioingia katika baadhi ya Nchi Duniani ambapo hadi sasa Zanzibar na Tanzania kwa Jumla hakuna maradhi hayo na kuelezea Tahadhari za kujikinga zilizochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na madawa na Vifaa vya kujikingia hafla iliofanyika ukumbi wa Wizara hio Mnazi mmoja Zanzibar

Nae Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk Fadhil Mohamed Abdalla aliwasisitiza  wananchi kuchukua  tahadhari kwa kufanya usafi kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kutia mkono, machoni, mdomoni na puani ili kujikinga na ugonjwa huo.

Mkurugenzi huyo alifahamisha dalili za maradhi ya corona ni kuwa na homa kali, mafua makali na joto kubwa mwilini pamoja na kutoweza kupumua hivyo jamii iendelee kudumisha usafi kwani ndio silaha ya afya.

Loading