MAAFISA WA ZFDA WAFANYA UKAGUZI WA MAENEO YA KUUZIA MAZIWA

Maafisa ukaguzi kutoka Wakala wa Chakula na Vipodozi Zanzibar wakifanya ukaguzi baada ya kutoa tangazo kwa wauza maziwa kuacha kutumia madumu na chupa za plastika kuhifadhia maziwa tangazo ambalo halijatekelezwa

Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeanza ukaguzi wa wauza maziwa wasiofuata utaratibu unaokubaliwa ikiwemo sehemu zisizo rasmi ili kulinda afya za wananchi.

Mkurugenzi Idara ya Udhibiti Usalama wa Chakula wa ZFDA Dk. Khamis Ali Omar alisema ukaguzi umefanyika baada ya kutoa elimu na matangazo kwa wauza maziwa kuacha kutumia chupa na madumu ya plastiki na katika maeneo yasiyo rasmi.

Alisema chupa na madumu ya plastiki baada ya kutolewa maziwa hayawezi kusafika na hubakisha chembe chembe za maziwa wakati wa kukosha ambazo baada ya muda huoza.

Dk. Khamis alisema zoezi hilo litakuwa endelevu na amewataka wauzaji wa maziwa kufuta maelekezo yanayotolewa na Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar ili kujiepusha na gharama zisizo za lazima.

Alisema chupa na madumu ya plastiki ambayo yamekuwa yakitumiwa na wauza maziwa hayapo salama na yanaweza kusababisha maradhi ya kuambukiza ikiwemo kifuakikuu.

Aliwashauri wauzaji wa maziwa kuwa na maeneo maalumu ya kuuza bidhaa hiyo kwa kutumia chupa za vigae zilizopunguzwa mwangaza na kutumia keni za aluminiam kubebea maziwa.

 Muuza maziwa wa eneo la Amani Haroun Abdalla alikiri kuwa  ZFDA walitoa elimu kuhusu madhara ya kutumia chupa na madumu ya plastiki lakini muda waliopewa kujitaarisha kutumia chupa za vigae na keni za alluminiam ni mfupi.

Alisema bei ya keni moja ya kubebea maziwa inagharimu zaidi ya shilingi laki mbili kiwango ambacho wauzaji wadogo waliowengi wengi hawawezi kumudu kununua kwa kipindi kifupi.

Muuzaji mwengine Ali Muhamed alisema tatizo kubwa liliopo Zanzibar hakuna kiwanda kinachozalisha chupa za vigae zinazotakiwa kutumika kwa ajili ya kuuzia maziwa.

Katika ukaguzi huo wafanyakazi wa ZFDA waliharibu lita kadhaa za maziwa waliyoyakuta yakiuzwa katika sehemu zisizo rasmi na kutumia chupa na madumu ya plastiki.

Loading